Serikali yapongezwa kwa kufanikisha ufadhili wa masomo vijana wanaotoka kaya maskini

NA JAMES K.MWANAMYOTO

MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo ameipongeza Serikali kwa kutoa ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kwa vijana wanaotoka katika familia maskini ambazo ni walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini ambao unaroatibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo akiongoza kikao kazi cha kamati yake jijini Dodoma kilicholenga kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Mhe. Chaurembo amesema, ufadhili huo unawawezesha vijana wanaotoka katika kaya maskini kupata elimu sawa na vijana wengine wanaotoka katika familia zinazojiweza kiuchumi.

Mhe. Chaurembo ameongeza kuwa, ufadhili huo unaotolewa na serikali kupitia TASAF licha ya kuzinufaisha kaya maskini, pia unaisaidia Serikali ya Awamu ya Sita kutimiza lengo lake la kuwapatia elimu bora watanzania wote bila kujali tofauti za kiuchumi walizonazo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akifafanua hoja za wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakati wa kikao kazi cha kamati hiyo jijini Dodoma kilicholenga kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Akizungumzia ufadhili huo unaotolewa na serikali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama, amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kutoa ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kwa vijana wanaotoka kaya maskini ambazo ni walengwa wa TASAF.

“Tuna mkataba na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu unaowawezesha vijana wote waliopata ufaulu mzuri wa kidato cha sita kupata ufadhili wa masomo ya elimu ya juu, na Mhe. Rais analifuatilia sana suala hili ili kusitokee yeyote aliyekidhi vigezo akakosa ufadhili,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu Kusini Unguja (CCM) Mhe. Mwantumu Dau Haji akichangia hoja wakati wa kikao cha kamati hiyo jijini Dodoma kilicholenga kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa mwaka wa fedha 2021/2022. 

Mhe. Jenista amesema, serikali inaamini kuwa vijana watakaopata ufadhili huo wa masomo ya elimu ya juu na kufanikiwa kuhitimu, watapata fursa ya kuajiriwa serikalini au kwenye sekta binafsi, hivyo watatoa mchango katika maendeleo ya taifa.

“Tunatarajia vijana hao wakihitimu ndio watakuwa watumishi wenye uadilifu na bidii ya kazi itakayosaidia kujenga uchumi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi,” Mhe. Jenista amefafanua. Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu anayewakilisha Vyuo Vikuu, Mhe. Dkt. Tea Ntala akichangia hoja wakati wa kikao cha kamati hiyo jijini Dodoma kilicholenga kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa ambaye pia ni Mbunge anayewakilisha Vyuo Vikuu, Dkt. Tea Ntala amesema amekuwa akipewa orodha ya vijana wanaoshindwa kumudu gharama za masomo ya elimu ya juu, hivyo ameomba awe anaiwasilisha orodha hiyo TASAF ili ijiridhishe kama vijana hao ni miongoni wa walengwa wanaostahili kupatiwa ufadhili.

“Mimi sina uwezo wa kufanya uchunguzi na kubaini kama vijana hao kweli wanatoka katika familia maskini au wanadanganya, japo wapo baadhi ya wakuu wa vyuo huniarifu kuwa vijana hao hawana uwezo wa kumudu gharama za masomo, hivyo naomba TASAF mshirikiane nami kuwawezesha wenye sifa stahiki kupata ufadhili,” Mhe. Ntala amesisitiza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Bw. Ladislaus Mwamanga akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi yake kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakati wa kikao kazi cha kamati hiyo jijini Dodoma kilicholenga kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022. 

Akitoa ufafanuzi wa ombi la Mhe. Tea Ntala, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Bw. Ladislaus Mwamanga amesema, wanafunzi wa vyuo vikuu wanaofadhiliwa na TASAF ni wale wanaokidhi kigezo cha kutoka katika kaya maskini, hivyo TASAF iko tayari kuwawezesha vijana hao iwapo itajiridhisha kuwa wanaotoka katika kaya maskini ambao ndio walengwa wa TASAF.

Bw. Mwamanga ameeleza kuwa, TASAF ina utaratibu mzuri wa kushirikiana na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu tangu mwaka 2017, utaratibu ambao umewezesha kutoa ufadhili wa masomo kwa vijana wengi wa vyuo vikuu wanaotoka katika familia maskini.

“Mwaka 2017 TASAF tuliwawezesha wanafunzi 277, mwaka 2018 na 2019 tuliwawezesha pia kupata mikopo, mwaka 2020 tuliwawezesha wanafunzi 872, mwaka 2021 tumewawezesha 1200 na kwa mwaka huu tuko kwenye hatua za mwisho kuwawezesha kupata mikopo,” Bw. Mwamanga amefafanua.

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umekuwa ni mkombozi wa kaya maskini nchini, licha ya kuziwezesha kaya hizo kiuchumi pia umetoa mchango mkubwa katika kuboresha huduma za kijamii katika sekta za elimu, afya, maji na miundombinu ya barabara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news