Rais Samia afanya uteuzi wa wenyeviti, watendaji

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa wenyeviti wa bodi na watendaji mbalimbali.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Oktoba 22, 2022 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bi.Zuhura Yunus.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mheshimiwa Rais Samia amemteua Dkt.Florens Martin Turuka, Katibu Mkuu mstaafu kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART).

Wakati huo huo,Mheshimiwa Rais amewateua maafisa watano kuwa wajumbe wa Bodi ya DART akiwemo Zainab Salome Msimbe, Mhasibu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhandisi Johansen Kahatano, Mkurugenzi wa Barabara, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (LATRA).

Pia, Mheshimiwa Rais Samia amemteua Bw.Aron Johnson Kisaka, Mkurugenzi wa Huduma za Usafirishaji, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi-Dodoma,Bw.Benjamini Kiloba Dotto, Mkurugenzi wa Miundombinu, Mamlaka ya ya Serikali Mtandao (eGA) na Bi.Mwantumu Mshirazi Salim, Katibu wa Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa Mauzo ya nje (Export Processing Zones Authorty - EPZA).

Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Samia amemteua, Bi.Beng'i Mazana Issa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa.

Bi.Beng'i ni Katibu Mtendaji, Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC). Baraza hilo ni taasisi ya Serikali iliyoanzishwa na Sheria ya 16 ya 2004 kama njia ya kuharakisha mchakato wa kuwawezesha Watanzania kiuchumi.

Aidha, Baraza lina majukumu ya kuwezesha kubuni, kupanga, kusimamia, kufuatilia na kutathmini na pia kuratibu shughuli zote za uwezeshaji wa kiuchumi nchini.

Pia linajukumu la kuhamasisha rasilimali na kusimamia fedha maalum kwa ajili ya shughuli za uwezeshaji wa kiuchumi.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Rais Samia amewateua maafisa watano kuwa Wajumbe wa Bodi ya Mikopo ya Serkali za Mitaa.

Walioteuliwa ni Dkt.Hemed Aziz Mpili, Afisa Ugavi Mwandamizi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI),Prof.Provident Jonas Dimoso, Makamu Mkuu wa Chuo wa Chuo Taaluma, Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) Dodoma na Bw.Said Abdallah Panga, Mkuu wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimali Watu, Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) Dodoma.

Wengine ni Bw.Joseph Felix Chilambo, Meneja Uendeshaji Biashara, Benki ya Maendeleo ya TIB Dar es Salaam na Bw.John Mihayo Cheyo, Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Ofisi ya Rais.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo kutoka kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, uteuzi huu wa Mheshimiwa Rais umeanza Oktoba 20, 2022.

Watendaji

Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Samia amemteua Prof.Tumaini Joseph Nagu kuwa Mganga Mkuu wa Serikali, kabla ya uteuzi huu, Prof.Nagu alikuwa Kaimu Mkuu wa Idara ya Tiba, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).

Prof.Nagu anachukua nafasi ya Dkt.Aifello Sichalwe ambaye atapangiwa kazi nyingine huku uteuzi wa Prof.Nagu kulingana na taarifa hiyo ukianza Oktoba 19, 2022.

Aidha, Mheshimiwa Rais Samia amemteua Bw.Deusdedit Kamalamo Bwoyo kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Wizara ya Maliasili na Utalii.

Bw.Bwoyo ambaye uteuzi wake umeanza Oktoba 20, 2022 kabla ya kuteuliwa alikuwa Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Misitu na Nyuki.

Pia, Mheshimiwa Rais Samia amemteua Bw.James Mahanga Sando kuwa Katibu Mtendaji wa Mamlaka ya Zabuni za Umma (Public Procurement Appeals Authority-PPAA).

Bw.Sando ambaye uteuzi wake umeanza Oktoba 20, 2022 kabla ya kuteuliwa alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Fedha katika Kampuni ya Crown Accounting and Consulting Firm jijini Dar es Salaam.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news