Simba SC yatinga Makundi Ligi ya Mabingwa barani Afrika

NA DIRAMAKINI

KLABU ya Simba ya jijini Dar es Salaam, Tanzania imefanikiwa kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika baada ya kuifunga Premiero De Agosto kutoka Angola bao moja katika mchezo uliopigwa leo.

Ni kupitia mtanange uliopigwa leo Oktoba 16, 2022 katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam,.

Simba SC wameingia katika hatua hiyo kwa jumla ya mabao 4-1 kufuatia ushindi wa 3-1 waliopata katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Novemba 11 nchini Angola wiki iliyopita.

Mchezo ulianza kwa kasi, Simba SC wakiliandama lango la De Agosto wakitafuta bao la mapema huku wakitengeneza nafasi kadhaa za kufunga, lakini hawatuzitumia vizuri.

Mshambuliaji kinara Moses Phiri awapatia bao la kwanza dakika ya 33 baada ya kupokea pasi ya Mohamed Hussein na kupiga shuti kali la chini chini lililomshinda mlinda mlango wa De Agosto.

Aidha, kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo dakika 10 za mwanzo De Agosto waliwashambulia mara kadhaa Simba SC, lakini hawakuweza kubadilisha kitu.

Kocha Juma Mgunda alifanya mabadiliko ya kuwaingiza Kibu Denis, Habib Kyombo, Gadiel Michael, Jonas Mkude na Erasto Nyoni na kuwatoa Pape Sakho, Augustine Okrah, Mohamed Hussein, Israel Patrick na Henock Inonga.

Post a Comment

0 Comments