Watumishi wa umma msiogope, semeni-Ndejembi

NA JAMES K. MWANAMYOTO

NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka watumishi wa umma nchini kutoogopa kuwasilisha changamoto zinazowakabili kwa kuwahofia waajiri kuwajengea chuki na kuwaahidi kuwa, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora itawalinda kwa sababu Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anataka kupata mrejesho utakaoiwezesha Serikali kuujenga Utumishi wa Umma wenye uadilifu na unaowajibika kwa masilahi ya taifa.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb) akitoa ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi kwa watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Lindi, Manispaa ya Lindi na wa taasisi za umma mkoani humo wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao kilicholenga kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.

Mhe. Ndejembi ametoa wito huo kwa watumishi wa umma nchini, wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Lindi, Manispaa ya Lindi, Halmashauri ya Wilaya ya Mtama na wa taasisi za umma mkoani Lindi.

“Sisi viongozi tunaomsaidia Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kusimamia Utumishi wa Umma tunapowatembelea msiogope kuelezea changamoto zinazowakabili kwani tunakuja kuzitatua, hivyo tutawalinda na iwapo mtaogopa mtajinyima fursa ya kuwasilisha changamoto zenu ili zitatuliwe kama Mhe. Rais alivyoelekeza,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Mhe. Ndejembi amesema Ofisi ya Rais-UTUMISHI haitosita kumchukulia hatua stahiki Afisa Utumishi au mwajiri atakayebainika kumuonea mtumishi aliyejitokea kuwasilisha changamoto zinazomkabili.

Akiwasilisha hoja kuhusu watumishi wa umma kupata changamoto ya kubadilishiwa miundo ya kiutumishi (recategorization), mmoja wa watumishi wa Idara ya Elimu Sekondari mkoani Lindi, Bw. Sharif Daudi Kiao amehoji ni kwanini mtumishi aliyejiendeleza kielimu kwa ajili ya kuutumikia umma pindi anapomuomba mwajiri kumbadilishia kada analazimika kushushwa mshahara wake ili apate sifa ya kukitumikia cheo kipya.

Akitoa ufafanuzi kuhusiana na hoja iliyowasilishwa na mtumishi huyo, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ametoa ushauri kwa watumishi wa umma nchini pindi wanapotaka kujiendeleza kielimu kuhakikisha wanazingatia uhitaji wa mwajiri kwa wakati huo ili wakihitimu wawe na tija kiutendaji ambayo inamshawishi mwajiri kumbadilishia kada (recategorization) ili aweze kutoa mchango katika Utumishi wa Umma.

Akizungumzia hoja ya mtumishi anayeomba kubadilishiwa kada kulazimika kushushwa mshahara wake, Mhe. Ndejembi ameeleza kuwa kwa watumishi wanaojiendeleza ndani ya kada zao kama vile Afisa Kilimo Msaidizi (Diploma) kuwa Afisa Kilimo (Degree) wakibadilishwa kada wanaombewa kibali cha mshahara binafsi, lakini kwa yule atakayeomba kubadilishiwa kada kwa ajili ya kukidhi matilaba binafsi (job satisfication) atalazimika kuanza na cheo cha kuingilia na mshahara wa cheo kipya kwa kada husika na atakuwa amekosa sifa ya kuombewa kibali cha mshahara binafsi.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi yuko mkoani Lindi kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku tatu, inayolenga kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma mkoani humo ikiwa ni pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news