Makamu wa Rais awauma sikio wananchi Tanga

NA DIRAMAKINI

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa wananchi mkoani Tanga kuhakikisha wanalinda amani iliyopo kwa kuwabaini na kutoa taarifa za wale wote wanaoingia katika mkoa huo kwa lengo la kufanya uhalifu.
Amesema hayo leo Novemba 20, 2022 mara baada ya kushiriki Ibada ya Misa Takatifu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Anthony wa Padua Jimbo Katoliki Tanga, ibada iliyoongozwa na msimamizi mkuu wa Jimbo hilo, Padre Thomas Kiangio.

Amesema, jografia ya mkoa huo inatumika kama njia ya kupokea watu mbalimbali ambao kati yao wapo wanaofanya uhalifu.

Pia Makamu wa Rais ametoa wito kwa waumini pamoja na wananchi wa Tanga kwa ujumla kuendelea na jitihada za kulinda mazingira ili kuepukana na athari zinazoendelea kujitokeza hivi sasa ikiwemo ukosefu maji pamoja na upungufu wa chakula.

Amewasihi viongozi wa dini kuendelea kuwasisitiza waumini juu ya maandiko matakatifu yanayoagiza kuilinda dunia ikiwemo kutunza mazingira.

Makamu wa Rais amewashukuru viongozi wa dini kwa kuendelea kuwa chachu ya amani iliopo nchini pamoja na kuwasihi kuendelea kuwaombea viongozi ili waweze kuongoza taifa kwa hekima ya Mungu.

Makamu wa Rais yupo ziarani mkoani Tanga ambapo anakagua shughuli mbalimbali za maendeleo pamoja na kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili wananchi wa mkoa huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news