Marekani yagonga msumari Makamu wa Rais wa Malawi kukamatwa kwa rushwa

NA DIRAMAKINI

UBALOZI wa Marekani nchini Malawi umesema unathamini juhudi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini Malawi (ACB) kufuatia kukamatwa kwa Makamu wa Rais, Saulos Chilima kwa tuhuma za kupokea hongo.

Chilima alikamatwa Novemba 25, 2022 baada ya kuhojiwa katika ofisi za ACB kwa madai kwamba alipokea hongo ya dola 280,000 kutoka kwa mfanyabiashara Zuneth Sattar rai wa Uingereza.

Katika taarifa yake, Ubalozi wa Marekani umesema unathamini juhudi za ACB kuchunguza na kufuatilia uwajibikaji katika kesi za rushwa.

“Hii inahitaji ujasiri na kujitolea kwa utawala wa sheria. Kesi hizi ni suala la mfumo wa mahakama wa Malawi, na tunahimiza mchakato wa haki, wa uwazi na unaofaa na mahakama kwa wale wote wanaotuhumiwa kwa uhalifu,” imesomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Pia Ubalozi wa Marekani umeitaka Serikali ya Malawi kuendeleza juhudi za kushughulikia suala la rushwa kwa kuwabaini, kuwafungulia mashtaka na kuwaadhibu wale wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa bila kujali itikadi za kisiasa au vyeo vyao.

Ubalozi katika taarifa hiyo umeeleza dhamira yake ya kuendelea kusaidia juhudi mbalimbali katika mapambano dhidi ya rushwa nchini Malawi.

Kilichojiri

Awali, Taasisi ya Kupambana na Rushwa nchini Malawi (ACB) ilidai kuwa, Makamu wa Rais Chillima alipokea kitita hicho cha fedha ili kumsaidia mfanyabiashara wa Uingereza, Zuneth Sattar kupata kandarasi za serikali ya Malawi.

“Kati ya Machi 2021 na Oktoba 2021, (Chilima) alipata faida ya fedha kiasi cha dola 280,000 na vitu vingine kutoka kwa Zuneth Sattar kama zawadi ya kusaidia Xaviar Limited na Malachitte FZE, ambazo ni kampuni zilizounganishwa na Zuneth Sattar kupewa kandarasi na serikali ya Malawi,”msemaji wa ABC alieleza Egrita Ndala.

Ndala alidai, Chilima alifikishwa mahakamani kusomewa mashtaka yanayomkabili akiwa ofisa wa umma kinyume na kifungu cha 24(1) cha Sheria ya Vitendo vya Rushwa ya Malawi kama inavyosomwa na kifungu cha 34 cha Sheria ya Vitendo vya Rushwa .

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Malawi, Chilima iwapo madai yake yatathibitishwa na mahakama, atakuwa anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 12 iwapo atapatikana na hatia ya makosa hayo.

Kifungu cha 396 cha Kanuni ya Adhabu ya Malawi kinasisitiza kwamba mtu mwenye hatia ya vitendo vya rushwa "atawajibika kwa kifungo cha miaka 12".

Mwezi Juni,mwaka huu iliripotiwa kuwa Rais Lazarus Chakwera aliacha kukasimu majukumu kwa Makamu wake, Chilima kufuatia madai ya hongo.

Mfanyabiashara Sattar ambaye alidaiwa kuwahonga zaidi ya maafisa 50 wa umma ili kupata kandarasi ambazo zilidaiwa kutumika kuilaghai serikali mabilioni ya kwacha, alikamatwa nchini Uingereza lakini bado hajafunguliwa mashtaka.

Wakati huo huo, Chilima ambaye ameshtakiwa kwa makosa sita ya rushwa, amepewa dhamana baada ya kufikishwa mahakamani jijini Lilongwe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news