MBOBEZI USAFIRI MAJINI

NA ADELADIUS MAKWEGA

MWISHONI mwa miaka ya 1980 mwanakwetu alikuwa na rafiki yake mmoja anayefahamika kama Joseph Maseke, rafiki yake huyu walikuwa wanalingana rika na wakati wa sikukuu kubwa kubwa za dini ya Kikristo kama vile Pasaka na Krisimasi ndugu hawa wawili walikuwa wanatumikia pamoja katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Antony wa Padua Mbagala Zakhem.

Na kwa kuwa walikuwa wadogo kazi yao kubwa ilikuwa ni kubeba mishumaa kutoka nayo Sakristia kwenda nayo Altareni misa inapoanza na kuibeba mishumaa hiyo kurudi nayo Sakristia wakati misa inapomalizika.
Kazi kubwa kubwa katika misa za kubeba chetezo, ubani, kubeba fimbo na kofia za Kadinali wakati huo hawakupewa ndugu hawa maana walikuwa wadogo mno kazi hizo zilikuwa za wakubwa na kwao ziliwazidi kimo.

Kuna siku kabla ya misa ya Krisimasi kusaliwa Joseph Maseke na mwanakwetu walifanya mazoezi na wenzao ya kutumikia na kujianda na sikukuu hiyo na kulikuwa na ujio wa kadinali Rugambwa walipofika Kanisani kuna sehemu ulikokwa moto wa chetezo cha misa hiyo, Joseph Maseke na mwanakwetu wakaambiwa wasitumikie misa hiyo, jambo hilo liliwaumiza sana ndugu hawa na kuanguka kilio wote wawili na wenzao kuingia Sakristia kuvaa kanzu na kutumikia, Joseph Maseke na mwanakwetu walipomaliza kulia walisali na kurudi nyumbani kwao salama salimini.

Mwanakwetu maisha ya urafiki wao yaliendelea, mwaka 1996 baba mzazi wa Joseph Maseke alikuwa mgonjwa sana na akalazwa Hospitali ya Tumbi Kibaha na akiwa hapo alitakiwa kufanyiwa upasuaji hivyo madaktari waliagiza mzee huyu atafute watu wa kumchangia damu kwa hiyo Mzee Maseke aliwajulishwa vijana wake akiwamo Joseph na kuifanya kazi hiyo vizuri sana.

Joseph akawajulisha vijana kadhaa wakaenda kutoa damu huko huko Tumbi wakitokea Mbagala maana familia yao ilikuwa inapendwa sana kwa sababu mbalimbali ikiwamo walikuwa wapenda sana michezo hasahasa soka akiwamo mjomba wao mmoja aliyefahamika kama Musa Lengulengu. 

Hospitali ya Tumbi waganga waliwaambia kuwa mchangiaji huyo lazima awe Kundi O la Damu (Universal Donor) kwa bahati mbaya siku ya kwanza walimpata mchangiaji mmoja tu kati ya watu 10 waliojitolea kwenda.

Joseph Maseke alijitahidi kurudi na kundi la kwanza akiwa mnyonge sana na alipokuwa anarudi alishuka Kituo cha Basi cha Mbagala Kizuiani na kupitia Uwanja wa Mpira wa Shule ya Msingi Mbagala yalipokuwa yanafanyika mazoezi ya timu mbalimbali za soka kila jioni. 

Akiwa anapita hapo uwanjani mwanakwetu akamuona Joseph Maseke akamtania akisema Padri mbona mnyonge, haujapewa Parokia? Joseph huku akitembea shingo yake imeinamia upande mmoja akajibu, “Mzee anaumwa, amelazwa Tumbi Kibaha, inahitajika watu wawili wakamchangie damu na leo hatukukamilisha zoezi hilo wanahitajika Univesal Donor wawili.”

Mwanakwetu akamjibu na kusema kuwa kaka hilo tu mbona dogo yeye ni Univesal Donor atakwewnda kutoa hiyo damu lakini hana nauli ya kutoka Mbagala hadi Tumbi Kibaha.

Joseph akamjibu mwanakwetu kuwa suala la nauli siyo shida,shida kwao ilikuwa ni kumpata huyo Univesal Donor.

Wakakubaliana wakutane hapo mapema ya asubuhi ya siku iliyofuata kwenda Tumbi Kibaha, kweli siku hiyo ilipofika walifanya hivyo na kupanda basi hadi Ubungo na hapo Ubungo hadi Kibaha na siku hii kulikuwa na kundi kubwa la watu kama kumi na hapo Hospitalini Tumbi vipimo vilifanyika na kupatikana Univesal Donor wawili akiwamo mwanakwetu. 

Wakachangia damu na kupewa kadi za utambulisho za uchangiaji wakiambiwa kuwa kadi hizo wakija siku yoyote kutibiwa waje nayo kuonesha kuwa waliwahi kuchangia damu Hospitali ya Tumbi.

Baba wa Joseph Maseke alifanyiwa upasuaji na kupona na kuruhusiwa kurudi nyumbani Mbagala na alipofika hapo aliagiza kutafutwa mwanakwetu ilikuwa tabu kumpata kwa sababu ya mambo ya shule lakini alipatikana na kufika mbele ya Mzee Maseke na mzee huyu kusema maneno haya,

“Mwanangu zamani kulikuwa na udugu wa kuchanjia damu, kitendo hicho klihusisha tone dogo japokuwa sasa kitendo hicho siyo salama kwa afya za binadamu lakini wewe umenichangia damu nyingi ili nifanyiwe upasuaji, nakushukuru sana kwa wema wako tambua kuwa wewe ni ndugu yangu na wanangu wote.”

Mwanakweu akanunuliwa soda akainywa na karanga zilizokaangwa na mama wa Joseph Maseke hapo hapo nyumbani kwa Mzee Maseke Mbagala Kwa Mangaya na alipomaliza aliwaaga na mwanakwetu kurudi zake nyumbani kwao.

Urafiki wa ndugu hawa hakutokea Kanisani tu bali ndugu hawa wawili kuishi jirani huko Mbagala kwa Mangaya na pia Joseph Maseke akiwa Shule ya Msingi Mbagala alisoma darasa moja na marafiki wengine wa mwanakwetu akiwamo dada mmoja aliyefahamika kama Rehema Mwinyimkuu (marehemu sasa), kumfahamu zaidi Rehema ni dada wa mwanamuziki Solo Thang-Ulamaa-Msafiri Kondo, urafiki wao ulikuwa imara sana ni urafiki wa udugu.

Joseph Maseke ambaye alitamani sana kuwa Padri tangu wakati huo lakini safari yake haikufikia lengo hilo, aligonga mwamba mwanzoni mwanzoni. Ndugu huyu kwa sasa ni mbobezi wa masuala ya usafiri wa majini (Marine Master). 

Kwa hilo mwanakwetu anaamini kuwa ule Upadri alioutamani Joseph Maseke anautimiza kwa namna nyingine huko huko katika Usafiri wa Majini.

“Niliwasiliana na brother Jose aliniunganisha na chuo cha ubaharini, nikajifunza na sasa ninafanya kazi na meli ya uvivu, ndiyo maana sionekani nyumbani.” Haya yalikuwa maelezo ya nahodha mmoja wa meli ya uvivu Mtanzania mzaliwa Mbagala alipozungumza na mwanakwetu.

Msomaji wangu inawezekana Marine Master ni msamiati mgeni sana kwa wasomaji wengi kwani wengi wetu tunafahamu juu ya nahodha(Captain). Ifahamike wazi kuwa Marine Master ni mkubwa zaidi kwani majukumu yake makuu ni matano;

“Kuhakikisha abiria wote wapo salama na mizigo yote ipo salama chomboni, ndiye anayepanga safari za meli, ndiye anayehakiksha sheria na kanuni za usafiri wa bahari zinafuatwa na kumbukumbu zote zinahifadhiwa vizuri, yeye ndiye anayehakikisha meli inafanyiwa ukarabati na matengenezo yote na pia ndiye anayesimamia masuala yote ya dharura ya usafiri wa majini baharini.”

Kwa sasa Joseph Maseke anafanya kazi na shirika moja kubwa la usafiri wa Bahari nchini Tanzania kwa nafasi hiyo hiyo ya MARINE MASTER.

Mwanakwetu kwa leo anaomba aishie hapo tu kwani amemkumbuka rafiki yake Joseph Maseke mbobezi wa masuala ya usafiri wa majini na pia anaikumbuka kadi yake aliyopewa ya uchangiaji wa damu mwaka 1996 ambapo yeye ameshaipoteza na anauliza je akienda Hospitali ya Tumbi watamkumbuka kuwa aliwahi kuchangia damu wakati huo?.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news