Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar laja na mikakati kabambe

NA MIZA OTHMAN

BARAZA la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ) limeona ipo haja ya kutumia mbinu mbadala ya kuwashawishi vijana katika kushiriki michezo mbalimbali, kwani kufanya hivyo kutaondokana na wimbi kubwa la vijana kujihusisha na vikundi viovu na kutapelekea kukuza maendeleo ya michezo nchini.

Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar, ndugu Mwalim Ali Mwalim ameyasema hayo wakati walipokuwa akizungumza na wajumbe wa baraza katika kikao cha kawaida cha robo ya pili cha Baraza la Michezo, kikao hicho kilifanyika katika Ukumbi wa Baraza la Mwanakwerekwe Wilaya ya Magharibi “B” Unguja.

Amesema, ni vyema Wajumbe wa Baraza hilo kuwa makini katika kutekeleza majukumu ya kazi zao, kwani kufanya hivyo kutasaidia kurahisisha usimamiaji na uendelezaji wa shughuli za michezo hapa Zanzibar.

Mwenyekiti huyo amesema, upo muhimu wa sekta ya michezo kupewa kipaumbele kwani sekta hiyo inasaidia kuwanyanyua vijana kuondokana na utegemezi katika kujikwamua kimaisha yao na kulinyanua taifa kiuchumi.

“Hakuna mtu yeyote anaweza kushawishiwa kuingia ndani ya michezo, kwani ni maamuzi ya mtu mwenyewe kushiriki mfano wachezaji kama Pele (marehemu), Beckham kutokana hivi sasa wanapata fursa za kushiriki maamuzi ya vikao mbalimbali katika taifa,"amesema Mwenyekiti.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar, Said Kassim Marine amesema Baraza la Michezo limeona upo umuhimu wa kuanzisha tamasha la michezo litakazoweza kuwainua vijana na kuonyesha vipaji walivyonayo kwa kuonekana ndani ya mataifa mbalimbali ulimwenguni.

Hata hivyo, amewataka wajumbe hao kushiriki katika vikao mbalimbali vinavyojadiliwa na kuweza kubuni mambo yatakayowawezesha kuibuwa njia za kukuza michezo hapa nchini.

Baadhi ya wajumbe walioshiriki katika kikao hicho wamesema ni vyema kuandaa kanuni na sheria na kufanyiwa kazi, kwani kufanya hivyo kutapelekea kurahisisha utekelezaji wa kazi zao kwa uhakika.

Post a Comment

0 Comments