Victoria Farming and Fishing Organization (VIFAFIO) yatoa mafunzo ya uongozi na utawala

NA FRESHA KINASA

SHIRIKA la Victoria Farming and Fishing Organization (VIFAFIO) lililopo Manispaa ya Musoma mkoani Mara limetoa mafunzo ya mifumo ya uongozi na utawala kwa wajumbe wa bodi ya shirika hilo pamoja na watumishi ili watambue majukumu yao kikamikifu katika kuleta ufanisi na tija.
Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kupinga ukatili uliozoeleka katika jamii unaotekelezwa na shirika hilo katika Halmashauri za Wilaya ya Musoma na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kwa ufadhili wa Shirika la Foundation for Civil Society ambao ulianza Septemba, mwaka jana.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika Februari 3, 2023 Meneja wa shirika hilo (VIFAFIO), Majura Maingu amesema, lengo ni kuhakikisha wanakuwa na uwezo na wanatambua wajibu wao na kuwa na uelewa madhubuti katika utekelezaji wa majukumu yao.
Maingu amesema, katika utekelezaji wa majukumu yao, VIFAFIO litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia na kuheshimu sheria, taratibu na kanuni za nchi ili kuendana na matakwa ya kuanzishwa kwake.

"Kupitia mafunzo haya, kwa hawa ambao tumekubaliana kuendesha hili Shirika tujue majukumu yetu vizuri katika kuihudumia jamii kwa kufuata sheria na taratibu za nchi,"amesema Maingu.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Makongo Maingu amesema kuwa, Bodi ya Shirika hilo ina wajibu wa kufanya kazi kwa kuongoza shirika kufikia malengo yake ikiwemo kuweka vipaumbele na malengo ya shirika na miongozo ya kupata rasilimali za kuendesha shirika, na kupitia na kutathimini utekelezaji wa mipango ya shirika hilo.

Aidha, amewahimiza kusimamia uwajibika wa bodi na sekretarieti kwa kuweka sera, miongozo na kanuni mbalimbali, kuhakikisha mikataba yote ya ubia inaendana na malengo na amali za shirika, kuhakikisha utekelezaji wa sheria na maagizo halali ya serikali na kusimamia matumizi ya rasilimali fedha.

Pia, amewaomba kusimamia na kutangaza heshima ya Shirika hilo ikiwemo ushiriki wa wajumbe wa bodi katika shughuli muhimu, kuimarisha Mawasiliano na watendaji, serikaki ngazi husika na jamii kwa ujumla pamoja na kuepuka maslahi mgangano.

Amewaasa pia, kuendeleza utamaduni wa kujifunza na kuelimishana kwa kushiriki kikamikifu katika fursa za mafunzo, kutoa taarifa za fursa na mafunzo zenye tija kwa Shirika pamoja na kujitolea kufundisha na kuwezesha wajumbe wa bodi na wadau wengine.
Upande wa Sekretarieti ya Shirika hilo chini ya Meneja wake ameiasa kuendelea kusimamia utekelezaji wa dira na dhana ya shirika ikiwemo kuongoza uandaaji na marekebisho ya mipango mkakati, sera na miongozo ya sera utekelezaji wa mwaka na kushirikisha wadau wote wa shirika wawe na uelewa mpana kuhusu dira na dhana.

Pia, kufanya usimamizi madhubuti wa rasilimali na fedha kwa kutathmini ubora wa kubuni na kupendekeza mabadiliko na kuandaa taarifa za fedha, kusimamia uandaaji wa bajeti ya mwaka na usimamizi wa shughuli za kila siku za shirika.

Kwa upande wake, Tendo Makori ambaye ni Mjumbe wa Bodi aliyeshiriki mafunzo hayo amesema, mafunzo hayo yatamsaidia katika utekelezaji wa majukumu yake na yamemsaidia kumuongezea ufanisi.
Mwenyekiti wa bodi ya Shirika hilo Costantine Sokanya (VIFAFIO) amesema, kupitia mafunzo hayo kila mmoja amepata upeo na maarifa thabiti ya kufanya kazi zao. Huku akisema shirika litaendela kubuni vyanzo vya mapato ili kuweza kutekeleza majukumu mbalimbali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news