Waonesha moyo wa shukurani kwa Prof.Muhongo

NA FRESHA KINASA

WANANCHI wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara wamempongeza Mbunge wao Prof. Sospeter Muhongo kwa kuendelea kushirikiana nao kwa dhati katika kuimarisha sekta ya elimu jimboni humo.
Wamesema Mbunge huyo amekuwa kiongozi bora katika kuonesha njia, kuwatia moyo, kuwapa hamasa na ushiriki wake wa moja kwa moja katika kuhakikisha sekta ya elimu inaimarika na kuleta mageuzi chanya ya kimaendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Wananchi hao wameyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati wakizungumza na DIRAMAKINI. Februari 3, mwaka huu.

"Nafurahi kuona juhudi za mbunge wangu Prof.Muhongo kwa ushiriki wake madhubuti wa kuchangia ujenzi wa maabara tatu za masomo ya sayansi katika Sekondari ya Seka. Masomo ya Sayansi yana umuhimu mkubwa sana katika kuleta maendeleo ya nyanja mbalimbali.

"Mbunge juzi katoa mifuko 150 ya saruji na pia kachangia chakula na vitabu, hajaanza jana ni kawaida yake kuchangia pia ni mhamasishaji namba moja kwa wananchi ili wasomeshe watoto na pia yeye binafsi kuchangia maendeleo moja kwa moja,"amesema Julius Bwire mkazi wa Seka.

Naye Veronica Mafuru mkazi wa Nyakatende amesema kuwa, Mheshimiwa Prof. Muhongo amekuwa daraja la kusaidia wanafunzi kupenda kusoma masomo ya Sayansi ikiwemo kutoa fedha zake kwa ajili ya kuchangia kuwalipa walimu wa masomo ya Sayansi na kuwaeleza umuhimu wa masomo hayo katika kukuza wataalam mbalimbali.

Sambamba na kuunga mkono kwa asilimia kubwa hatua ya Serikali kwa kupata wasomi bora wa sayansi watakaokuja kulisaidia taifa na jamii kwa ujumla.

"Tunaendelea kuona Mbunge akifanya kazi ya kuendesha harambee mbalimbali jimboni mwetu, alifanya harambee ya ujenzi wa Sekondari ya Muhoji katika Kata ya Bugwema hivi karibuni. Pia alitoa michango yake mingi tu na pia namna ambavyo anatuunganisha wananchi na Serikali kuhakikisha sekta ya elimu inaleta matokeo chanya.

"Mbunge hapendi kuona watoto wanatembea umbali mrefu ndio maana anakuwa na mikakati ya kujenga shule mbili kwenye baadhi ya kata ili watoto wasipate shida na wazazi wanaitikia kwa mwitiko chanya,"amesema Veronica Mafuru.

"Seka ameendesha harambee kila harambee michango yake ndio mikubwa hutoa kiwango kikubwa. Wananchi mara nyingi sisi michango yetu ni kidogo tofauti na nguvu kazi. Yeye amekuwa akitoa pesa kusaidia kuwalipa walimu wa Sayansi hii yote inaonesha shabaha yake kuona wasomi wengi wanaandaliwa kwa faida yetu na hapendi matokeo mabaya na ndio maana mkazo wake ni kuona watoto wanapata ufaulu mzuri,"amesema Mwajuma Mathias.

Naye Maira Faustine Mkazi wa Muhoji amesema,Prof. Muhongo husaidia mahitaji ya shule watoto hasa wanaokwenda kujiunga na masomo ya kidato cha tano ambao wazazi wao hawana uwezo ikiwemo kuwanunulia mahitaji mbalimbali na kuwapa nauli jambo ambalo amesema mbali na kuwa jema, lakini anatimiza vyema amri ya upendo ambayo Mungu ameiagiza katika vitabu vitakatifu vya dini yaani Biblia na Quran.

"Hivi karibuni tumesikia Mbunge Prof.Muhongo atafanya kikao na wakuu wa shule zote 27 za sekondari zilizopo kwenye jimbo letu la Musoma Vijijini ambacho kitalenga kujadili "Mapendekezo ya uboreshaji wa kujifunza na kufundisha katika Sekondari zetu. Hii ni hatua nzuri sana kwani ninaamini kikao hicho kitakuwa na maazimio mazuri yenye tija na mikakati madhubuti ya kukuza ufaulu kwa shule zetu,"amesema na kuongeza kuwa.

"Nakumbuka pia Mbunge Prof. Muhongo alishawahi kufanya Konganano la Elimu lilifanyika Songe Sekondari Mjini Musoma wakati Adam Malima akiwa ni RC wa Mara, kama sio mwaka jana ni mwaka juzi.

"Wadau wa elimu walijadili mambo muhimu sana baada ya mkoa wetu kutokuwa na matokeo mazuri. Hakika Prof.Mubongo nia yake thabiti ni kuona elimu inakuwa na faida katika kuleta mabadiliko chanya,"amesema Pius Maigwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news