Kenya yachukua hatua kukabiliana na Marburg

NA DIRAMAKINI

SERIKALI ya Jamhuri ya Kenya kupitia Wizara ya Afya imetangaza kuchukua hatua za haraka kukabiliana na mlipuko wa Virusi vya Marburg ambavyo vimeripotiwa huko mkoani Kagera, Tanzania.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Afya katika Wizara ya Afya Kenya, Dkt.Patrick Amoth kupitia taarifa aliyoitoa leo Machi 22, 2023 amesema,Wakenya wanapaswa kuwa waangalifu na kuzingatia dalili zinazohusiana na virusi hivyo ili kuepuka madhara.

Pia, Serikali imebainisha hatari inayoweza kusababishwa na mabasi ambayo yanavuka mpaka na watu wanaovuka mipaka kupitia maeneo ya mpaka wa Kenya na majirani zake.
 
Zinazohusiana
 
 
Dkt.Amoth alizitaja Sirare na Isebania miongoni mwa miji iliyowekwa katika hali ya tahadhari kutokana na msongamano wa magari ya watu na magari yanayoingia mataifa jirani kupitia maeneo ya mpakani yaliyotengwa.

"Mji huu unahudumiwa na Uwanja wa Ndege wa Bukoba na vivuko vya mara kwa mara kwenda na kutoka Mwanza ambavyo vina uhusiano na Kisumu nchini Kenya.

"Kuna idadi ya mabasi ambayo hufanya safari kati ya Bukoba na Kampala nchini Uganda kila siku na baadhi yake huishia katika maeneo fulani nchini Kenya,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.

Machi 21, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Afya nchini Tanzania, Mheshimiwa Ummy Mwalimu amesema uchunguzi wa Maabara ya Taifa umethibitisha uwepo wa virusi vya Marburg ambavyo vinasababisha ugonjwa wa Marburg Virus Disease (MVD) katika Mkoa wa Kagera.

Ni ambao umesababisha vifo vya watu watano hadi sasa ambapo amesema ugonjwa huo hauna tiba mahususi bali hutibiwa kwa dalili anazokuwa nazo mgonjwa.

“Uchunguzi ambao tumeufanya katika Maabara yetu ya Taifa ya Afya ya Jamii umethibitisha uwepo wa virusi vya Marburg ambavyo vinasababisha ugonjwa unaojulikana kama Marburg Virus Disease(MVD).

“Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa huu wa Marburg uligundulika kwa mara ya kwanza Ujerumani mwaka 1967 katika Mji wa Marburg na ndio asili ya jina la ugonjwa huu, ugonjwa huu ulishawahi kuripotiwa katika Nchi mbalimbali za Afrika na Ulaya.

“Ugonjwa huu huambukizwa kutoka kwa binadamu mmoja kwa mwingine hususani kwa njia ya kugusa majimaji ambayo yanaweza kuwa mate, mkojo, damu, machozi au kinyesi yatokayo kwenye maiti au mgonjwa mwenye dalili, maambukizi pia yanaweza kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu iwapo mtu atakula au kugusa mizoga au wanyama walioambukizwa,”alifafanua Waziri Ummy Mwalimu.

Awali, Serikali kupitia Wizara ya Afya ilitoa tahadhari juu ya uwepo wa ugonjwa ambao bado ulikuwa haujajulikana mkoani Kagera katika Wilaya ya Bukoba Vijijini ambapo watu saba walisadikika kupata dalili za homa, kutapika, kutokwa damu maeneo mbalimbali ya mwili na figo kushindwa kufanya kazi na watu watano kati yao wakaripotiwa kufariki.

Katika hatua nyingine, Wizara ya Afya nchini Kenya imewahakikishia wananchi kuwapa taarifa za mara kwa mara na kwa wakati zinazohusu kuenea kwa virusi hivyo na njia mbalimbali za kukabiliana nao.

"Tayari Kenya imeanzisha utaratibu wake wa ufuatiliaji na kuimarisha ufuatiliaji katika maeneo yote ya mpaka kati ya Kenya, Tanzania na Uganda,"ameongeza Dkt.Amoth.

Pia, Serikali imewataka Wakenya kuripoti dalili zozote zinazoonekana kuhusiana na virusi hivyo kwenye kituo cha afya ili kutathminiwa na kudhibitiwa mapema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news