Kwa nini kanisa la Askofu Dkt.Ceasar Masisi limetakiwa kusitisha huduma?

NA DIRAMAKINI

KANISA la Spirit Word Ministry linaloongozwa na Askofu Dkt.Ceasar Masisi na mkewe huko Ukonga Stakishari Polisi jijini Dar es Salaam limesitisha huduma zake baada ya kupokea notisi.

"Shalom wana wa Mungu, leo tarehe 9.03.2023 Spirit Word Ministry imepokea NOTISI ya maelekezo kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ambapo NOTISI hiyo pamoja na malekezo mengine imeielekeza taasisi ya Spirit Word Ministry kusitisha shughuli zote za uendeshaji wa taasisi mara moja mpaka pale taasisi itakapopewa maelekezo mengine na mamlaka hiyo.

"Kufuatia maelekezo hayo, Spirit Word Ministry inawatangazia watu wote kuwa imesitisha shughuli zake zote ikijumuisha ibada, ratiba za madarasa ya Jumapili au siku yoyote ile, katika matawi yote ya Spirit Word Ministry madarasa ya mitandao ya kijamii kama Whatsapp na Telegram.

"Vipindi vilivyokuwa vikiruka kupitia mitandao ya kijamii na TOP TV na shughuli zingine zote ambazo zimekuwa zikiendeshwa na huduma ya Spirit Word Ministry.Kusitishwa huku kutaendelea mpaka pale taasisi itakapopata maelekezo mengine kutoka kwa mamlaka husika.Katika Kristo ni salama sana,"imeeleza sehemu ya taarifa hiyo kutoka katika uongozi wa Spirit Word Ministry.

Hivi karibuni, huduma hiyo imekuwa ikitoa mahubiri ambayo yamesababisha mkanganyiko mkubwa katika jamii huku pia yakiibua maswali mengi kwa Watanzania ambao wanathamini, kuheshimu na kuzingatia kwa kina maadili, mila na tamaduni za Kitanzania.

Ni mafundisho ambayo pia yalikuwa yanaenda kinyume na imani pamoja na misimamo thabiti ya Wakristo kama ilivyo katika Biblia Takatifu, rejea...Walawi 18:22, 24-25. “Usilale na mwanamume mfano wa kulala na mwanamke; ni machukizo.

"Msijitie unajisi katika mambo hayo hata mojawapo; kwa maana hizo taifa nitakazozitoa mbele zenu zimekuwa najisi kwa mambo hayo yote; na hiyo nchi imekuwa najisi; kwa ajili ya hayo naipatiliza uovu wake juu yake, na hiyo nchi yatapika wenyeji wake na kuwatoa.”

Ukilitafakari kwa kina neno hilo la Mungu, unaweza kuona kuwa mojawapo ya sababu ya kufutiliwa mbali kwa mataifa yaliyoimiliki Kanaani ni kwa sababu ya dhambi kadha wa kadha ikiwemo mapenzi ya jinsia moja.

Aidha, Mungu anawaonya Israel kuwa nchi itawatapika watu watendao mambo mfano wa hayo, taifa linalotenda mambo ya jinsi hiyo au kuruhusu mambo ya jinsi hiyo linajiweka katika wakati mbaya na mgumu wa hukumu ya Mungu.

Kwa sababu, Mungu hulifuta au kumfuta mtu awaye yote anayetenda machukizo ya kiwango hiki cha kushiriki mapenzi ya jinsia moja.

Mapenzi ya jinsia moja au ushoga huitia nchi unajisi na kuiharibu ardhi au nchi ikilaaniwa inawatapika watu wake yaani inawakataa, inawaua kwa sababu iliumbwa kwa ajili ya utukufu wa Mungu, wakati wowote dunia inapohukumiwa ni lazima tuelewe inasababishwa na aina hii ya uovu pamoja na maovu mengine.

Rejea,...1Wakoritho 6:9-10, “Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi.”

Unaweza kuona, maandiko katika Agano la Kale na Agano Jipya yamerejea kwa wingi kwa kina na kwa upana na urefu katazo la Neno la Mungu kuhusu aina hii ya uovu duniani.

Sote tunapaswa kufahamu kuwa,mapenzi ya jinsia moja kwa mujibu wa maandiko ni dhambi, Mungu yuko kinyume kabisa na mapenzi ya jinsia moja kwa sbababu ni kinyume na mapenzi yake na mpango wake wa uumbaji.

Vile vile, mapenzi ya jinsia moja yanaharibu kabisa mfumo wa mwanadamu kimwili, kiroho na kiuadilifu, lakini pia unaharibu kabisa mpango mzima wa Mungu kuhusu tendo la ndoa ambalo Mungu amelikusudia lifanyike katika utakatifu na utaratibu uliowekwa na Mungu chini ya baraka ya kuzaliana na kuongezeka.

Kwa mujibu wa maandiko dhambi ya ushoga inachukua nafasi ya juu kabisa ya dhambi ambazo ni machukizo kwa Mungu, Biblia inakemea kwa ukali zaidi suala hili katika maandiko.

Rejea,...Mambo ya Walawi 18:22-24, “Usilale na mwanamume mfano wa kulala na mwanamke; ni machukizo. Wala usilale na mnyama ye yote, ili kujitia unajisi kwake; wala mwanamke asisimame mbele ya mnyama ili kulala naye; ni uchafuko.

"Msijitie unajisi katika mambo hayo hata mojawapo; kwa maana hizo taifa nitakazozitoa mbele zenu zimekuwa najisi kwa mambo hayo yote.”

Rejea,...Mambo ya Walawi 20:13, “Tena mtu mume akilala pamoja na mtu mume, kama alalavyo na mtu mke, wote wawili wamefanya machukizo; hakika watauawa; damu yao itakuwa juu yao.”

Wakati huo huo, ni jukumu letu wazazi na walezi kuhakikisha tunayapa malezi ya watoto nafasi ya kwanza ili kifanya familia, jamii na Taifa kuwa salama na kukaa mbali na matendo maovu ambayo yamechipukia kwa kasi.

Kumekuwa na visa mbalimbali vya mmomonyoko wa maadili katika jamii huku sababu kubwa zikielekezwa kwa wazazi na walezi kushindwa kusimamia vyema makuzi ya watoto wao.

Tutambue kuwa,Mungu/Mwenyezi Mungu ametoa jukumu na wajibu kwa wazazi kuwapa watoto malezi bora yatakayowawezesha kuwa watu wema katika jamii.

Malezi ya wazi hayaanzii baada ya kuzaliwa, malezi bora huanzia mtoto anapokuwa tumboni mwa mama mpaka kufikia umri wa kujitegemea.

Aidha, malezi ya mtoto yamegawanyika katika sehemu kuu mbili, malezi ya kimwili na malezi ya kiroho.

Malezi ya kimwili ni yale yote anayofanyiwa mtoto ili akue katika afya njema. Malezi haya huanza mara tu mama anapopata ujauzito. Baba ana wajibu wa kumtunza mke kwa kumpatia vyakula maalumu ili mama na mtoto aliyeko tumboni wawe na afya nzuri.

Hata baada ya mtoto kuzaliwa wazazi husika wanapaswa kumlea mtoto kimwili na kimaadili kwa kuwafunza tabia na mwenendo mwema unaomridhisha Mungu/Mwenyezi Mungu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

  1. Ni sawa kabisa ufungiwe tu, ni aina gani ya ibada unayoifanya hapo kanisani kwako, kiukweli haina utukufu hata kidogo, tumekuvumilia sana kama miongoni mwa wakiristo, huwezi sema waandishi wa biblia eti ni washenzi alafu wakati huo unaitumia hyo biblia, alafu nyimbo mnazoimba hazina baraka kabisa, Mungu hadhihakiwi kamwe!

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news