Simba, Yanga SC zawapa raha Watanzania

NA DIRAMAKINI

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho barani Afrika nyota zao zimezidi kung'ara.
Ni kutokana na Yanga SC kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kwenda Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Real Bamako ya Mali katika mchezo wa Kundi D.

Ni mtanage uliopigwa Machi 8, 2023 katika Dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Mabao ya Yanga SC yalifungwa na mshambuliaji, Fiston Mayele dakika ya nane na Jesus Moloko dakika ya 68, huku Yanick Bangala akikosa penalti dakika ya 57.

Mechi ya Kundi D iliyotangulia jijini Tunis nchini Tunisia, wenyeji Monastir walishindwa 1-0 dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Sasa Monastir inaendelea kuongoza Kundi D kwa alama zake 10, ikifuatiwa na Yanga SC kwa alama saba,TP Mazembe alama tatu na Real Bamako alama mbili.

Mechi zijazo Machi 19, mwaka huu Yanga SC watakuwa wenyeji wa Monastir jijini Dar es Salaam na Real watawakaribisha TP Mazembe jijini Bamako.

Katika hatua nyingine bao la kiungo Mzambia, Clatous Chama dakika ya 45 liliipa Simba SC ushindi wa 1-0 dhidi ya Vipers ya Uganda katika mchezo wa Kundi C Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ni kupitia mtanage wa nguvu ulipopigwa katika Dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Ushindi huo umeifanya Simba SC ifikishe alama sita na kusogea nafasi ya pili, nyuma ya Raja Casablanca yenye alama 12 na mbele ya Horoya yenye alama nne na Vipers alama moja baada ya wote kucheza mechi nne.

Aidha, ushindi huo umerejesha matumaini ya Simba SC kwenda robo fainali ya michuano hiyo kuelekea mechi mbili za mwisho dhidi ya Horoya jijini Dar es Salaam siku ya Machi 18,mwaka huu na Raja Casablanca nchini Morocco Machi 31,mwaka huu.

Aidha, baada ya mchezo huo, Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ aliwasifia wachezaji kwa jitihada kubwa walizofanya kufanikisha ushindi huo.

Robertinho alisema haikuwa mechi rahisi kwa kuwa, Vipers walikuwa wanawapa presha mara kwa mara, lakini wachezaji wao walikuwa makini muda wote.

Kocha Mkuu huyo aliongeza kuwa, walicheza kwa umoja kuanzia kwa walinzi, viungo hadi kwa washambuliaji na ndicho kilisababisha ushindi upatikane.

“Nawapongeza wachezaji wangu kwa jitihada walizofanya, tumecheza kwa umoja kuanzia nyuma hadi mbele hilo ndilo jambo zuri.

“Kwenye Ligi ya Mabingwa hakuna mechi rahisi hata sisi tulijipanga kwa hilo kutoka kwa Vipers, kinachotakiwa ni kupata pointi tatu,”alisema Robertinho.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news