Rais Dkt.Samia afanya mabadiliko mawaziri, manaibu na makatibu wakuu

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri na Makatibu Wakuu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Agosti 30, 2023 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt.Moses M.Kusiluka, katika mabadiliko hayo,Rais Dkt.Samia ameanzisha nafasi ya Naibu Waziri Mkuu na kuifuta Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Baada ya hatua hiyo, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameunda wizara mpya mbili ambazo ni Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Uchukuzi.

Pia, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameimarisha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kuongeza nafasi ya Naibu Waziri na Katibu Mkuu watakaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki.

Katibu Mkuu Kiongozi amefafanua kuwa, katika mabadiliko hayo,Rais Dkt.Samia amemteua Naibu Waziri Mkuu, mawaziri wanne, naibu mawaziri watano, makatibu wakuu watatu na naibu makatibu wakuu watatu.

Vile vile amewabadilisha wizara baadhi ya mawaziri na makatibu wakuu ambapo mabadiliko hayo ni kama ifuatavyo;
 
Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amemteua, Dkt.Doto Mashaka Biteko kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati. Katika nafasi ya Naibu Waziri Mkuu atakuwa anashughulikia Uratibu wa Shughuli za Serikali.

Kwa upande wa uteuzi wa mawaziri na naibu mawaziri, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amemteua Jerry William Silaa, Mbunge wa Jimbo la Ukonga kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mheshimiwa Peter Mavunde, Naibu Waziri wa Kilimo ameteuliwa kuwa Waziri wa Madini huku Mheshimiwa Prof.Makame Mnyaa Mbarawa aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ameteuliwa kuwa Waaziri wa Uchukuzi.
 
Aidha, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amemteua Innocent Lugha Bashungwa, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kuwa Waziri wa Ujenzi.

Naye, Mheshimiwa Godfrey Msongwe Kasekenya aliyekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchakuzi ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi.

Huku, Mheshimiwa Alexander Pastory Mnyeti, Mbunge wa Jimbo la Misungwi akiteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Kilimo.

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amemteua, Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini kuwa Naibu Waziri wa Uchukuzi.

Vile vile, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amemteua Judith Salvio Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum mkoani Ruvuma kuwa Naibu Waziri wa Nishati.

Mheshimiwa Dustan Luka Kitandula, Mbunge wa Jimbo la Mkinga ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maliasilia na Utalii.

Uhamisho wa Mawaziri na Naibu Mawaziri

Wakati huo huo,Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amemhamisha Mheshimiwa January Yusuf Makamba kutoka Wizara ya Nishati kwenda kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Aidha, Mheshimiwa Stergomena Lawrence Tax amehamishwa kutroka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwenda kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Naye, Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa amehamishwa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii kwenda kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI).

Huku, Mheshimiwa Angellah Jasmine Kairuki akihamishwa kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) kwenda kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa, Dkt.Damas Daniel Ndumbaro amehamishwa kutoka Wizara ya Katiba na Sheria kwenda kuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Kwa upande wake, Mheshimiwa Balozi Dkt.Pindi Hazara Chana amehamishwa kutoka Wizara ya Utamaduni, sanaa na Michezo kwenda kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.

Naye Mheshimiwa Stephen Lujwahuka Byabato amehamishwa kutoka Wizara ya Nishati kwenda kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki atakayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki.

Uteuzi makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu.

Kupitia taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi imefafanua kuwa, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amemteua Prof.Godius Walter Kahyarara aliyekuwa Katibu Tawala Mkoa wa Geita kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi.

Pia, Mhandisi Cyprian John Luhemeja aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu).

Naye Balozi Prof.Kennedy Gastorn ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki atakayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki.

Dkt.Ally Possi aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Uchukuzi) ameteuliwa kuwa Naibu katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi.

Ludovick Nduhiye aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Ujenzi) ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi na Mhandisi Mwajuma Juma Waziri ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji.

Uhamisho wa makatibu wakuu

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amemhamisha Prof. Jamal Adam Katundu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira, na Wenye Ulemavu) kwenda kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Maji.

Dkt.Seif Abdallah Shekalaghe amehamishwa kutoka Wizara ya Afya kwenda kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.

Vile vile, Dkt.John Anthony Jingu amehamishwa kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwenda kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya.

Aidha, kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt.Moses M.Kusiluka uteuzi huu unaanza leo Agosti 30, 2023 na viongozi walioteuliwa wataapishwa Septemba Mosi, 2023 Ikulu Ndogo, Zanzibar saa 5:00 asubuhi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news