Serikali yataka rasilimali fedha makao ya watoto zitumike vizuri

DAR ES SALAAM-Wamiliki wa Makao ya Watoto wametakiwa kuhakikisha wanatoa huduma kwa mujibu wa sheria na kanuni na kuhakikisha rasilimali zinazopatikana kwa ajili ya kusaidia watoto zinatumika kikamilifu kwa maendeleo na ustawi wa watoto. 
Hayo yamesemwa Agosti 4,2023 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe.Dkt.Dorothy Gwajima wakati akifungua Mkutano wa Wamiliki wa Makao ya Watoto Mkoa wa Dar es Salaam.
Dkt.Gwajima amebainisha kwamba, pamoja na makao mengi kufanya kazi nzuri na kwa uwazi, baadhi yamekuwa yakikusanya rasilimali na kujinufaisha wao zaidi kuliko walengwa ambao ni watoto walioko kwenye vituo hivyo.

Huku wamiliki wa baadhi ya makao hayo wakiwazuia na kuwapa vitisho Maafisa Ustawi wa Jamii pale wanapofika kwenye makao hayo kufanya ufuatiliaji na ukaguzi wa utoaji wa huduma. 
"Jambo hilo ni kosa kisheria kwa mujibu wa Kifungu cha 146 (2) (c) na adhabu yake ni kifungo kisichopungua mwaka mmoja au faini isiyopungua milioni mbili na isiyozidi milioni 10 au vyote viwili na pia Ofisi ya Msajili inaweza kufuta leseni ya kumiliki makao,"amesema Dkt.Gwajima.

Amewataka wamiliki wa makao hayo kuwaruhusu bila vipingamizi Maafisa Ustawi wa Jamii kuingia makaoni na kufanya ukaguzi wakati wowote inapohitajika.
Akisisitiza kuhusu hatma ya huduma kwa mtoto aliyeko kwenye makao, Dkt.Gwajima amesema, kila mmiliki wa makao anatakiwa kuhakikisha watoto anaowalea wananufaika na huduma za makao na kuandaliwa kuunganishwa na familia au jamii kupitia Malezi ya Kambo au Kuasiliwa na au kuwezeshwa kujitegemea kwa wale waliofikia umri na kujengewa uwezo. 

Aidha, Dkt.Gwajima ametoa siku 90 kwa wamiliki wa makao ya watoto kote nchini kuhakikisha wanahuisha Kamati za Makao na miezi sita kwa kila mwenye makao kuwa amekamilisha taratibu zote za umiliki na uendeshaji wa makao, vinginevyo wawasiliane na wizara moja kwa moja iwapo watakumbana na changamoto.
Katika hatua nyingine, Dkt.Gwajima amewapongeza na kuwatia moyo wanaoendesha Makao ya Watoto kwa kufuata taratibu za uendeshaji na kuongeza kuwa, wizara inakamilisha Mapitio ya Mwongozo wa Uanzishaji na Uendeshaji wa Makao ya Watoto na inatarajia kutoa toleo jipya Septemba 2023 ili kuimarisha ulinzi wa watoto kwa kila nyanja. 
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt.John Jingu amesisitiza wamiliki wa vituo hivyo kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za usajili na uendeshaji wa makao na kwamba, wizara itaimarisha ufuatiliaji wa makao yote nchini ambayo kwa sasa yako jumla 431 huku 58 yakiwa Mkoa wa Dar es Salaam.
Nao wamiliki wa makao ya watoto Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Bw. Evans Tegete wamepongeza juhudi za Serikali za kuwa na jukwaa la pamoja la mawasiliano na Serikali ambalo litawasaidia kwenda pamoja kwenye kuboresha hatua za maendeleo na ustawi wa watoto wa kwenye makao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news