Simamieni mapato ya ndani kuboresha kilimo, mifugo na uvuvi-Waziri Mkuu

MBEYA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ihakikishe kuwa mapato yatokanayo na mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi yanatengwa na yanatumika katika sekta husika kulingana na miongozo iliyopo ili kuboresha sekta hizo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama ufugaji wa kisasa wa samaki aina ya Sato wakati alipotembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika maonesho ya wakulima ya kimataifa Nanenae kwenye uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya, Agosti 3, 2023.

“Ofisi ya Rais (TAMISEMI) hakikisheni mnasimamia Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2023/2024 unaozitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga mapato ya ndani yatokanayo na tozo mbalimbali kwenye mazao ya kilimo (asilimia 20), mifugo (asilimia 15) na uvuvi (asilimia 5) zinarudi na kutumika kuboresha sekta hizo ikiwa pamoja na uendelezaji wa mazao ya kimkakati,” alisema.

Alitoa wito huo Agosti 3, 2023 wakati akizungumza na wadau na washiriki mara baada ya kukagua mabanda ya Maonesho ya Nane Nane Kitaifa yanayoendelea kwenye viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.

Ili kuimarisha uzalishaji wa mazao ya kilimo, uvuvi na mifugo, Waziri Mkuu aliwataka wadau wa sekta hizo wazitumie taasisi za fedha zilizopo nchini kupata mikopo itakayowasaidia kuongeza tija na kuendeleza biashara zao.

“Taasisi za fedha zimefungua dirisha kwa ajili yenu, wanataka wawasikie. Hakuna maendeleo bila kukopa, lakini ni lazima vigezo na masharti vizingatiwe. Unapotaka kufanya maendeleo ukakosa mtaji, nenda kakope lakini ukikopa mwisho wake lazima urejeshe ili na wengine waweze kukopa.”

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali imeendelea kufanya mazungumzo na taasisi mbalimbali za fedha ili ziweze kushusha riba kwenye mikopo wanayotoa na kuongeza fursa kwa wajasiriamali nchini ili wapate mikopo na kuendeleza shughuli zao ziweze kuwa na tija. “Nimefurahi sana kukuta baadhi yao wameshusha riba mpaka asilimia tisa. Ni matumaini yangu watashuka zaidi,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwaagiza Wakuu wa Mikoa na viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa washirikiane na wizara husika kuhakikisha vijana wanapatiwa maeneo ya mashamba, mafunzo na kuwatafutia wadau watakaowasaidia kupata mitaji ya kuendesha shughuli za kilimo, mifugo, uvuvi na masoko ya uhakika.

“Ninawaagiza Wakuu wa Mikoa mshirikiane na Mamlaka ya Serikali za Mitaa katika maeneo yenu kuhakikisha wanatenga maeneo ili vijana wanaopata mafunzo ya BBT (mpango wa kuwawezesha vijana kulima, kufuga na kuvua samaki kibiashara) wakute yako tayari. Tunataka hawa vijana wakitoka kwenye mafunzo, wakute maeneo yako tayari na waanze kazi mara moja,” alisisitiza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news