Tanzania, Ujerumani kuendeleza ushirikiano

DAR ES SALAAM-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema serikali za Tanzania na Ujerumani zimekubaliana kuwa na mazungumzo ya ushirikiano wa maendeleo yatakayofanyika mwaka 2024.
Serikali hizo zimeagiza timu za wataalam kutoka pande zote mbili kuendelea kuwa na mazungumzo ya mara kwa mara yanayolenga kuimarisha ushirikiano na kubainisha maeneo mapya yenye umuhimu kwa nchi zote.

Rais Samia amesema hayo Oktoba 31, 2023 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kumpokea na kuzungumza na Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani,Dkt. Frank Walter Stainmeier ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.

Aidha, Rais Samia ameeleza kuwa Tanzania iko tayari kufungua majadiliano kuhusu yaliyopita kwenye historia ya Utawala wa Ujerumani nchini ambapo mojawapo ni urejeshaji wa mabaki yaliyopo kwenye makumbusho mbalimbali za Ujerumani kwa familia zao.

Rais Samia amesema anatambua juhudi za pamoja zinazofanywa na taasisi za Serikali hizo mbili zinazolenga kufanikisha azma hiyo ikiwemo pia kuwajengea uwezo wataalam na kuongeza uwezo wa makumbusho za Tanzania na Ujerumani.

Rais Samia pia ameishukuru Ujerumani kwa namna inavyounga mkono Tanzania kwenye miradi ya maendeleo hususan sekta za afya, maji, kilimo, elimu, utalii,utamaduni, michezo, ulinzi, maliasili, uhifadhi wa mazingira na udhibiti wa fedha.

Kuhusu uwekezaji, Rais Samia amesema viongozi wote wawili wamekubaliana na kusisitiza mchango muhimu wa biashara na uwekezaji katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news