Mfumo wa NeST waokoa shilingi bilioni 13.33 ununuzi wa karatasi za zabuni

NA GODFREY NNKO

MFUMO wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Kielektroniki (NeST) umeokoa shilingi bilioni 13.33 za Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/24 ambazo zingetumika katika ununuzi wa karatasi kwa ajili ya maandalizi na ukamilishaji wa zabuni.
Hayo yamesemwa leo Mei 12,2025 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dennis Kwame Simba katika kikao kazi kati ya wahariri, wanahabari chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).

NeST ni mfumo ambao umeundwa na wazawa hapa nchini ambao ni mbadala wa mfumo wa awali wa manunuzi ya umma uliojulikana kama Tanzania National e-Procurement System (TANePS).

"Sheria ya Ununuzi wa Umma Sura Namba 410 ya mwaka 2023 imeipa PPRA mamlaka ya kuanzisha na kusimamia Mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa njia ya Mtandao (e-Procurement System) ili kurahisisha uchakataji wa zabuni za umma kupitia mfumo.

"Mfumo wa NeST (National e-Procurement System of Tanzania) ni mfumo wa ununuzi wa umma kwa njia ya mtandao unaosimamiwa na PPRA chini ya Wizara ya Fedha, ukiwa na lengo la kuongeza uwazi, uwajibikaji, na ufanisi wa ununuzi wa umma kupitia teknolojia ya kisasa."

Simba amesema, mfumo ulianza kutumika rasmi Julai 1, 2023 na ulizinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Septemba 9, 2024 akiwakilishwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Dotto Biteko (Mb) kupitia hafla ya Kongamano la Ununuzi wa Umma la Afrika Mashariki lililofanyika mkoani Arusha.

Pia amesema kuwa, tangu kuanza kutumika kwa mfumo wa NeST, inakadiriwa kuwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 pekee utafiti wa awali uliofanywa na mamlaka umebaini kuwa matumizi ya mfumo huo yamesaidia kupunguza tani 617.85 za utoaji wa kaboni angani.

"Na mfumo huu umepunguza muda unaotumiwa na taasisi nunuzi kupata taarifa za wazabuni, hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa muda wa uchakataji wa zabuni."

Simba ameongeza kuwa, uwepo wa nyaraka za zabuni ndani ya mfumo umesaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza muda uliokuwa unatumiwa na taasisi hizo wakati wa kuandaa nyaraka za zabuni.

Mbali na hayo, Simba amesema kuwa,katika taasisi nunuzi zote, jumla ya taasisi nunuzi 57,993 zimesajiliwa NeST zikiwa na jumla ya watumiaji 117,900 ambao wamesajiliwa katika mfumo.

"Katika taasisi nunuzi hizo, kuna taasisi kuu na kasimiwa 1,215 na taasisi za ngazi za chini za serikali za mitaa 56,778. Aidha, watumiaji 53,584 wamesajiliwa kama wasimamizi wa wazabuni."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news