Kambi ya upasuaji mtoto wa jicho Iringa kuwafikia watu zaidi ya 700

IRINGA-Watu wapatao 120 katika siku ya kwanza wamefikiwa na huduma ya upasuaji wa mtoto wa jicho katika kambi ya matibabu ya ugonjwa huo inayoendeshwa na waataalam wa afya ya macho wakiwemo madaktari bingwa wabobobezi kutoka hospitali za Nyanda za Juu Kusini katika kituo cha Afya Isimani mkoani Iringa.
Kambi hiyo inayoendelea kwa siku saba katika kituo hicho inatarajia kufanya upasuaji kwa watu kati ya 600 hadi 700 kwa siku sita baada ya watu wengi kujitokeza kutoka maeneo ya Iringa Vijijini na maeneo jirani kuchangankia huduma hiyo inayotolewa na Serikali kwa ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Hellen Keller.

Akiongea mara baada ya kufanyiwa usuaji wa ugonjwa wa mtoto wa jicho,Bi. Nuru Mathias Kayage, amesema amekuwa akiishi na ugonjwa huo tangu mwaka 2021 hali ambayo imechangia kuvunjika kwa ndoa yake kutokana na kuwa na uoni hafifu, lakini sasa amekuwa na matumaini mapya baada ya kuanza kuona upya kufuatia tiba ya upasuaji wa mtoto wa jicho.
‘’Nimepitia kipindi kigumu mpaka ndugu jamaa na marafiki walikuwa wananitenga hata nilipokuwa nawatembelea ndugu walikuwa wanadhani naenda kuomba msaada, kutokana na changamoto hii nilitelekezwa na mume nikiwa na watoto watatu, sijui niwashukuru vipi walioleta msaada huu, sina cha kuwalipa, Mungu awabariki sana,’’ amesema Bi. Matiasi.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James akiukaribisha ujumbe wa Bodi ya Wataalam kutoka Hellen Keller Ofisini kwake amelishukuru shirika hilo kwa kutoa msaada wa vifaa kila vinapoitajika, kutoa utaalam kwa madaktari wenyeji na kuendeleza ushirikiano kati yao na Serikali.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema, lengo la ujumbe wa Hellen Keller mkoani Iringa ni kujionea namna gani huduma wanazofadhili zinavyofanya kazi ikiwemo kujadiliana kwa pamoja maeneo mengine ya ushirikiano kwani shirika hilo limekuwepo hapa nchini kwa zaidi ya miaka 30.

Naye Rais wa shirika hilo duniani,Sarah Bochie ameuambia ujumbe wa Mkuu wa Mkoa wa Iringa kuwa shirika lake liko mkoani Iringa ili kujionea huduma zinazotolewa kwa vitendo kwani shirika lake linafanya kazi kwa kanzi data na takwimu ili kutoa tathimini ya huduma zake.
Ujumbe huo kabla ya kwenda mkoani Iringa Agosti 4, 2025 ulikutana na Menejimenti ya Wizara jijini Dodoma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news