NA LWAGA MWAMBANDE
NI wazi kuwa, kupata fedha halali ni msingi muhimu wa uadilifu binafsi na ustawi wa kijamii.
Kwani,mapato yanayopatikana kwa njia halali hujenga imani, huimarisha uwajibikaji, na huchangia maendeleo endelevu ya kiuchumi.
Aidha,katika muktadha wa kitaaluma, tafiti zinaonesha kuwa jamii zinazothamini uhalali wa kipato hupunguza vitendo vya rushwa, huongeza tija kazini, na huimarisha usawa wa kijamii.
Pia, fedha halali huwezesha mipango bora ya kifedha, hutoa amani ya kisaikolojia, na huongeza mchango chanya wa mtu kwa familia na taifa kwa ujumla.
Kwa kutambua mchango wa imani katika maadili ya kazi, mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa,ni vyema pia kumtukuza Mungu kwa wema wake unaoongoza juhudi za binadamu.
Lwaga anabainisha kuwa,shukrani kwa Mungu huimarisha unyenyekevu na uaminifu, huku zikihimiza matumizi yenye hekima ya rasilimali zilizopatikana kwa haki.
Kwa mtazamo huu, Lwaga Mwambande anasema kuwa, kupata fedha halali si tu wajibu wa kisheria na kimaadili, bali pia ni tendo la kumheshimu Mungu kwa kuishi kulingana na misingi ya haki, bidii na uaminifu ikiwa ni nguzo zinazochochea maendeleo ya mtu na jamii kwa ujumla. Endelea;
1. Pesa sabuni ya roho, kwa mtu hata taifa,
Hata ukitaka hoho, bila pesa wewe lofa,
Mwenye pesa ana joho, hata aso maarifa,
Jitahidi pata pesa, uweze kuheshimika.
2. Mtu aliye na pesa, anacheza kama refa,
Macho huwa yamnasa, na kummwagia sifa,
Kwa watu awa asusa, wamuimba ni mshefa,
Jitahidi pata pesa, uweze kuheshimika.
3. Unapotafuta pesa, zisijefanya ukafa,
Uhalali ukasusa, uharamu uwe sifa,
Hapo mimi nakuasa, taishia uwe lofa,
Jitahidi pata pesa, uweze kuheshimika.
4. Kuna watu wana pesa, ila waishi kilofa,
Kwa sababu hizo pesa, kufuru kwao ni dhifa,
Wengine wamewatesa, wakae kwenye masofa,
Jitahidi pata pesa, uweze kuheshimika.
5. Ulozi kupata pesa, utabakia ni lofa,
Mashariti hizo pesa, ndugu wanaweza kufa,
Usitake hizo pesa, ukayaleta maafa,
Jitahidi pata pesa, uweze kuheshimika.
6. Jambazi hizo si pesa, wengine wanapokufa,
Mtaani ukitesa, laana kwa walokufa,
Tafuta halali pesa, kwa watu tapata sifa,
Jitahidi pata pesa, uweze kuheshimika.
7. Wizi kazini na pesa, huwezi kuwa mshefa,
Kutakasisha si pesa, haramu hata kwa FIFA,
Kazi ya halali pesa, huwezi pata kifafa,
Jitahidi pata pesa, uweze kuheshimika.
8. Hapa duniani pesa, hazitoshi hadi kufa,
Upatazo hizo pesa, hayo ni yako masafa,
Ridhika na zako pesa, usitake za Zulfa,
Jitahidi pata pesa, uweze kuheshimika.
9. Zakupa kibali pesa, ipokee taarifa,
Zinakuinua pesa, ukaribishwe kwa dhifa,
Mahitaji ya kisasa, kuyakosa ni ulofa,
Jitahidi pata pesa, uweze kuheshimika.
10. Ila ukipata pesa, Mungu umpe wadhifa,
Zisijekufanya pesa, ukajikweza kwa sifa,
Nyenyekea hasa hasa, akuinue masafa,
Jitahidi pata pesa, uweze kuheshimika.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
