NA DIRAMAKINI
MWAKA 2025 ukiwa ukingoni, ni kumbukizi ya miaka 64 ya Uhuru wa iliyokuwa Tanganyika, hivi sasa ni Tanzania. Hapana shaka kuwa mojawapo ya mafanikio makubwa zaidi ya taifa ni kuimarika kwa Sekta ya Maji inayohudumia wananchi na kubadilisha maisha yao kila kila kukicha. Pamoja na changamoto za hapa na pale kazi inafanyika kwa kasi kukidhi mahitaji ya wananchi.


Sehemu ya mradi wa maji wa miji 28, ukiwa ni mradi mkubwa wa maji wa kimkakati unaotekelezwa na serikali ukiwa katika hatua za mwisho ili kuwafikia wananchi eneo la Mangaka wilaya ya Nanyumbu mkoa wa Mtwara.
Sio siri, ni safari na hatua ya kutoka kwenye visima vya enzi za Mkoloni na maji yasiyo salama hadi ujenzi wa mabwawa, mitambo ya kutibu maji na ulazaji wa mabomba katika kila kona ya nchi, kwa miradi mikubwa na midogo, na mitambo ya kisasa ya kuchimba maji ili kuwafikia wananchi nchi nzima, Serikali ya Tanzania imebadilisha upatikanaji wa maji kuwa chachu ya maendeleo na fursa.
Baada ya Uhuru wa mwaka 1961, Sekta ya Maji ilikuwa changa, isiyo na mpangilio na kwa kiasi kikubwa ilihudumia miji ya kiutawala, kwa mpango wa Mkoloni.
Mpango huo haukuweka kipaumbele kwa jamii nyingi za maeneo ya vijijini na mijini, ambapo Watanzania wengi walitegemea mito, mabwawa na visima vidogo vilivyochimbwa kwa mikono.
Upatikanaji ulikuwa wa muda mfupi, wanawake na watoto walitumia muda mrefu kutafuta maji, jambo lililopunguza fursa za kujiendeleza kwa elimu na kazi za uchumi.
Katika miongo iliyofuata, mipango ya maendeleo iliweka mkazo kupanua huduma, lakini ni katika miaka 20 iliyopita ambapo sekta ya maji imetanuka zaidi na imepata mabadiliko makubwa zaidi.
Mabadiliko haya yalikuja kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP), ambapo tayari awamu mbili zimekamilishwa na Serikali na ya tatu utekelezaji wake unaendelea.
Mpango huu wa kitaifa umejikita katika nguzo nne ambazo ni: usimamizi wa rasilimali za maji, usambazaji wa maji vijijini, usambazaji wa maji mijini na usafi wa mazingira; na uimarishaji wa taasisi na mifumo.
Upangaji wa pamoja, mageuzi ya kisheria na miradi ya kimkakati ilivutia wadau wa maendeleo chini ya maono ya kitaifa ”kuhakikisha kila Mtanzania anapata majisafi, salama na ya uhakika”.
Hadi mwezi Desemba 2023 jumla ya miradi ya maji 374 iliyogharimu kiasi cha fedha ya Tanzania shilingi 128,177,655,882 ilikuwa imekamilika. Wakala wa Usambazaji Maji Vijijini (RUWASA) inaendelea na utekelezaji wa miradi 1,172 iliyobaki ili kutimiza azma ya Serikali ya kutoa huduma ya uhakika ya majisafi na salama kwa maeneo ya vijijini.
Matokeo yanaonekana wazi, ambapo upatikanaji wa maji vijijini umeongezeka hadi zaidi ya asilimia 83 kufikia Desemba 2024. Mabadiliko haya yametokana na kutekelezwa na kukamilika kwa miradi zaidi ya 2000.
Wanawake na watoto wameacha zile safari ndefu za kutafuta maji, wanafunzi wanaweza kuzingatia masomo yao, na kaya zinawekeza muda katika shughuli za kiuchumi. Changamoto zipo na maeneo ambayo hayajafikiwa kwa uhakika yanafanyiwa kazi na hayajaachwa ambapo mitambo ya serikali ya kuchimba maji imenunuliwa seti 25 mahsusi kwa jukumu hilo.
Eneo la Maji mijini pia limepata kuimarika zaidi na mageuzi makubwa. miji kama Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza, Arusha (Mradi wa Jiji la Arusha), Tanga, Kigoma, Morogoro na Mbeya imeshamiri kwa ujenzi wa miradi mipya, uboreshaji na upanuzi wa mtandao wa kusambaza maji, vituo vya kusafisha maji, mabomba makuu. Kutokana na miradi hiyo na mingine mingi, kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji kimeongezeka na kufika asilimia 91.6 mwezi Desemba 2024.
Makao makuu ya nchi, Dodoma imefanyika kazi kubwa, mojawapo ikiwa ni ujenzi wa Mradi wa Maji wa Nzuguni kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa maji na upanuzi wa mtandao wa kusambaza maji, huku mkoa wa Mwanza ukinufaika na uwepo wa maji ya uhakika ya Ziwa Victoria kupitia miradi ya Butimba, Sengerema na miradi mingine ya maji na usafi wa mazingira mijini na vijijini ambapo mamia ya maelfu ya wakazi wamepata huduma, hatua hiyo imesaidia kaya, vituo vya kutolea elimu, vituo vya huduma za afya na maeneo biashara kunufaika.
Aidha, miradi mikubwa ya Nzega-Igunga-Tabora, Mugango-Kiabakari-Butiama (Mara), Same-Mwanga-Korogwe (Kilimanjaro), Orkesumet (Manyara), Bugoro–Lugata na Mwadubina–Manguluma (Mwanza), miji sasa inatoa huduma ya majisafi na salama kwa wakazi wa maeneo hayo.
Kwa upande wa maeneo yaliyokuwa na uhaba wa huduma za maji kutokana na kutokuwa na vyanzo vya uhakika, miradi mikubwa kutoka vyanzo vya uhakika imetekelezwa na mingine inaendelea kutekelezwa.
Moja ya miradi ya kisasa na mikubwa zaidi ni Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Simiyu, uwekezaji wa takribani shilingi bilioni 440 kwa fedha kutoka mfuko wa Green Climate Fund, Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW), na Serikali ya Tanzania unaendelea.
Mradi huu unachukua maji kutoka Ziwa Victoria kwa kuhudumia makao makuu ya mkoa wa Simiyu na wilaya zake pamoja na vijiji 103 vilivyoko pembezoni mwa bomba kuu umbali wa kilomita 12 kila upande ukitarajiwa kuongeza upatikanaji wa majisafi kwa wakazi wa vijijini na mijini.
Mradi umefiki asilimia 70 ya utekelezaji wake mpaka sasa, ni mfano mikakati ya Serikali kuimarisha huduma ya maji kwa kuzingatia mabadiliko ya tabianchi na mahitaji mbalimbali ya msingi katika jamii.
Mradi huu unatarajia kunufaisha takribani wananchi zaidi ya 495,000 kwa kuwapatia majisafi na salama, kuboresha huduma za usafi wa mazingira pamoja na kukuza mbinu bora na endelevu za kilimo katika jamii zinazolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Utekelezaji wa mradi huu unahusiana moja kwa moja na malengo ya Maendeleo endelevu ya ya Sekta ya Maji nchini Tanzania na mikakati ya kimataifa ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Pamoja na hayo, upatikanaji wa fedha umeimarika kwa kuanzishwa kwa Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF) ili kutoa rasilimali fedha zinazotumika kwenye utekelezaji wa miradi ya maji nchini pamoja na kuimarika kwa Diplomasia ya Uchumi kati ya Tanzania na mataifa rafiki duniani, wadau wa maendeleo nao wameendelea kufadhili miradi nchini.
Mikakati bora inayozingatia uwekezaji unaendana na maono ya taifa ikiwemo Sera ya Maji ya Taifa Dira ya Maendeleo 2050 pamoja na ongezeko kubwa la Bajeti ya Serikali kwenye Sekta ya Maji zimeweza kuvutia uwekezaji wa Sekta za Umma na Binafsi, zikisaidia ukuaji endelevu wa sekta. Aidha, maboresho ya Mifumo ya kiteknolojia ikiwemo Mfumo Mama wa Utoaji Huduma za Maji Kimtandao (MAJIIS) kwa Wataalam wa Sekta ya Maji.
Vilevile suala la elimu halijaachwa nyuma, Chuo cha Maji kimezidi kuimarishwa na kuongeza upatikanaji wa wataalam wa Sekta ya Maji sanjari na kujenga uwezo wa wataalam mbalimbali katika sekta. Hivyo, kuimarisha utendaji wa watumishi na kuongeza ufanisi wa kazi.
Serikali inaendelea kuchukua hatua kutatua changamoto mbalimbali za sekta, ikiwemo kupunguza kiwango cha upotevu wa maji, kuimarisha huduma kwa wateja, ikiwemo matumizi ya teknolojia ya kisasa, kuimarisha huduma ya majisafi na majitaka mijini na vijijini ili kukidhi ukuaji wa haraka na ongezeko la watu na kulinda vyanzo vya maji ikiwa ni moja ya baadhi ya vipaumbele vya sasa.
Mabadiliko ya tabianchi ni changamoto pia, na hivyo kuhitaji uwekezaji katika miundombinu bora na imara, pamoja na uendeshaji na matengenezo ya miradi ili iweze kuwa endelevu.
Lakini mafanikio halisi ni maisha yaliyobadilika katika jamii. Miongoni mwake ni mwananchi kuchota maji nyumbani na hata wasio nayo nyumbani kutotembea zaidi ya mita 400 kwenda kuyachota; shule na zahanati kuwa na huduma ya uhakika ya maji ili kuhudumia jamii; wafugaji na wakulima kupata maji ya uhakika kwa ajili ya kazi za msingi; jamii zinaboresha usafi, afya na fursa za kiuchumi.
Maji, zaidi ya sekta nyingine yoyote, hubadilisha uhuru kuwa heshima, afya na fursa halisi kwa kila mwananchi popote pale alipo.
Takwimu za Serikali mpaka Desemba 2024 zinaonesha ukuaji huu. Katika miaka minne ya hivi karibuni kwa uongozi wa Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, miradi ya maji 2,331 imekamilika kati ya hiyo 1,965 vijijini na 366 mijini.
Aidha, miradi mikubwa inayotarajiwa kutekelezwa ni pamoja na Gridi ya Maji ya Taifa ikilenga kutumia vyanzo vya maji vya uhakika kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kutoa maji katika maeneo yenye wingi wa maji kupeleka katika maeneo yenye upungufu.
Pia, miradi mingingine mikubwa inatekelezwa ikiwa katika hatua mbalimbali; Mradi wa maji wa Miji 28, Mabwawa ya Farkwa kwa Dodoma, na Kidunda kwa mikoa ya Pwani, Dar es salaam na Morogoro ambalo litakuwa muarobaini wa upungufu wa huduma ya maji katika hayo maeneo, na mto Kiwira kwenda Mbeya.
Mafanikio haya yameongeza upatikanaji wa huduma ya maji vijijini na mijini, kuboresha ushirikiano kati ya wadau na kuimarisha taasisi za sekta ya maji na sekta nyingine.
Kadri tunavyoadhimisha miaka 64 ya uhuru, Sekta ya Maji inasimama kama ishara ya mafanikio, mipango na ahadi kwa wananchi.
Inaonyesha nguvu ya kupanga kwa muda mrefu, uwekezaji mkakati na utashi wa kisiasa. Sura inayofuata ni wazi: kufikisha huduma ya maji katika vijiji vyote, kuimarisha mitandao ya majisafi na majitaka mijini; kusimamia, kuendeleza, kulinda na kutunza vyanzo vya maji na kuboresha utoaji wa huduma (Service Delivery) kwa sababu miradi imekamilika na inatakiwa kuhudumia wananchi kwa sasa na vizazi vijavyo.
Pia, kuimarisha uendeshaji na matengenezo ya miradi, kuongeza vyanzo vya mapato na uendelevu wa huduma Kwa kutumia mbinu hizi, Tanzania inaweza kuhakikisha majisafi, salama na ya uhakika hayawi tu huduma, bali ni nguzo ya ustawi wa taifa.
Inapoadhimishwa Siku ya Uhuru, taifa linapoinua bendera yake, pia linainua kiwango cha maisha ya wananchi wake kwa rika zote; ushahidi kwamba uhuru haupo tu kwenye historia, bali unajengwa kila kunapo pambazuka, katika kila tone la maji yanayofika kwenye nyumba, shule, zahanati na mashamba kote nchini kwa mabadiliko ya maisha wananchi kusonga mbele zaidi.