MORONI-Ubalozi wa Tanzania umeratibu utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Softnet Technologies Comores na ANADEN, wakala wa maendeleo ya kidijitali nchini Komoro, kwa lengo la kuimarisha mtaji wa rasilimali watu, kuboresha miundombinu ya kidijitali, na kuinua fahirisi ya maendeleo ya taifa.
MoU hiyo ilisainiwa na Bw. Maharage Chande (Softnet) na Bw. Mouinou Ahamada (ANADEN). Akizungumzia ushirikiano huu, Bw. Chande alisema:
“Tunataka Softnet Technologies Comores na ANADEN ziwe kituo cha ubora katika mageuzi ya kidijitali barani Afrika katika ukanda wa nchi zinazozungumza kifaransa.”
Ushirikiano huu utalenga kufundisha wataalamu wa ndani, kuhamisha ujuzi wa kiteknolojia, na kuhakikisha kwamba wataalamu wa ICT, wahandisi na tekinolojia wa Komoro wana uwezo wa kutekeleza na kudumisha miradi ya kidijitali kwa uhuru, kukuza umiliki wa ndani na endelevu.
Kupitia ushirikiano huu, uzoefu wa kikanda wa Softnet na uongozi wa kitaasisi wa ANADEN unatarajiwa kuimarisha miundombinu ya kidijitali ya Umoja wa Komoro na kuharakisha mageuzi ya kidijitali ya taifa








