DAR-Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bi. Sauda Msemo, amekutana na ujumbe wa Shirikisho la Mikopo ya Nyumba la Ulaya (European Mortgage Federation-EMF) ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mikopo ya Nyumba Tanzania (TMRC), Bw. Oscar Mgaya, kwa lengo la kujadiliana kuhusu fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta ya mikopo ya nyumba nchini.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika leo Januari 9,2026 katika Ofisi za Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam, Bi. Msemo alisema kuwa, ili kuendelea kuchochea ukuaji wa sekta ya mikopo ya nyumba, bado kuna haja ya kuongeza upatikanaji wa mikopo yenye gharama nafuu, hatua itakayowawezesha wananchi wengi zaidi kumiliki nyumba na hivyo kuchangia ustawi wa kijamii na kiuchumi wa nchi.
Aidha, Bi. Msemo alieleza kuwa Benki Kuu itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi katika kuboresha mazingira ya upatikanaji na utoaji wa mikopo ya nyumba, hususan kupitia kuimarisha mifumo ya kifedha, kuhimiza uwekezaji na kuimarisha uhimilivu wa sekta ya fedha kwa ujumla.






