Rais Dkt.Mwinyi aongoza maziko ya marehemu Joseph Abdallah Meza

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi leo Januari 31,2026 amewaongoza viongozi mbalimbali wa Serikali, Chama Cha Mapinduzi pamoja na wananchi katika maziko ya marehemu Joseph Abdallah Meza, yaliyofanyika Kisauni, Mkoa wa Mjini Magharibi, majira ya alasiri.
Marehemu Joseph Abdallah Meza alifariki dunia tarehe 29 Januari 2026 alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam.
Katika uhai wake, marehemu Meza aliitumikia nchi kwa uadilifu na kujitoa katika nyadhifa mbalimbali za Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), zikiwemo Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), Kamishina wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) kabla ya kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), pamoja na kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC).

Marehemu alizaliwa tarehe 8 Agosti 1959 na amefariki tarehe 29 Januari 2026, akiwa ameacha mjane na watoto saba.

Akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya familia, mtoto wa marehemu, Paulina Joseph Meza, amemshukuru Rais wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa upendo, msaada na mchango mkubwa alioutoa katika matibabu ya marehemu, na kumuelezea marehemu kuwa alikuwa mtu wa watu, mwenye moyo wa upendo na mshikamano.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaungana na familia, ndugu, jamaa na wananchi wote katika kuomboleza msiba huu mkubwa. "Bwana ametoa na Bwana ametwaa, jina la Bwana lihimidiwe.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here