KIGOMA-Ujumbe wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ukiongozwa na Waziri wa Nchi, anayeshughulikia masuala ya Ustawi wa Jamii, Hatua za Kibinadamu na Mshikamano, Mhe. Eve Bazaiba Masudi umetembelea Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu mkoani Kigoma.
Mhe. Masudi ametembelea kujionea maisha ya Wakimbizi wa DRC katika kambi hiyo na kusikiliza maombi na mapendekezo yao kwa Serikali ya DRC.
Akizungumza na wakimbizi katika uwanja wa mikutano kambini hapo, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kutoa hifadhi kwa Wakimbizi kutoka nchini DRC katika hali ya utu na amani kwa takribani miaka 30 tangu kuanzishwa kwa kambi hiyo.
Aidha, amewaeleza kuwa Serikali ya DRC inaendelea na jitihada za kutafuta suluhisho la kuleta amani ya kudumu ili waweze kurejea nchini kwao.
Pia amewasihi kuishi kwa nidhamu na maadili ili kuilinda heshima ya DRC na kuthamini ukarimu wa Serikali ya Tanzania.
Mhe. Masudi amewataka Wakimbizi walio tayari kurejea nyumbani kuendelea kujiandikisha rasmi ili waweze kurejea kwenye makazi yao na kufanya shughuli za maendeleo, mambo ambayo hawawezi kufanya wakiwa kambini.
Naye, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. James Millya (Mb) amewaeleza wakimbizi hao kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kusimamia misingi ya Sheria za Kimataifa za uhifadhi wa Wakimbizi hivyo, itaendelea kushirikiana nao katika kipindi chote wawapo nchini pamoja na kuwahakikishia usalama wao katika mchakato mzima wa kurejea nchini kwao. Aidha, ameeleza kuwa zoezi la kurejea nyumbani ni la hiari na si shuruti.
Akiwasilisha taarifa ya kambi, Kaimu Mkuu wa Kambi ya Nyarugusu, Bw. Samwel Kuyi ameeleza kuwa kambi ina jumla ya wakimbizi 132,404. Wakimbizi 86,918 ni kutoka DRC, 45,346 ni Warundi na 98 kutoka mataifa mengine. Zaidi ya 60% ya wakimbizi wa DRC ni watoto chini ya miaka 18 kati yao 21,660 ni watoto chini ya miaka mitano.
Moja ya wakimbizi, Apolina Masumbuko amesema wako tayari kurejea nyumbani na kuomba Serikali ya DRC iweze kurejesha amani nchini kwao ili warudi katika mazingira salama na tulivu.


















