Askari jela miaka miwili kwa kusababisha kifo cha Nashon Kiyeyeu

IRINGA-Mahakama Kuu Kanda ya Iringa imemhukumu Askari Polisi namba F.4987, Sajenti Rogers Mmari, anayefanya kazi katika Kituo cha Polisi Ipogolo, kutumikia kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia ya kusababisha kifo cha kijana Nashon Kiyeyeu.
Hukumu hiyo imetolewa na Jaji Angaza Mwipopo, aliyesema kuwa mahakama imeridhika pasipo shaka yoyote kwamba mshtakiwa alihusika na tukio hilo baada ya kuchambua ushahidi wa pande zote.

Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, tukio hilo lilitokana na taarifa iliyotolewa na mwananchi, Beatrice Kimata, aliyedai kuwa marehemu aliiba simu yake. Baada ya kupokea taarifa hiyo, Sajenti Rogers alimtafuta kijana huyo na alipompata alianza kumpiga akimshinikiza kurejesha simu hiyo.

Mahakama ilisikia kuwa kipigo hicho kilisababisha majeraha makubwa kwa marehemu hadi kupoteza fahamu. Baadaye alipelekwa katika hospitali binafsi kwa matibabu, lakini hali yake iliendelea kuwa mbaya na kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Iringa, ambako alithibitishwa kufariki dunia.

Aidha, mahakama ilibaini kuwa licha ya madai ya wizi, mshtakiwa hakuwahi kufungua kesi rasmi dhidi ya marehemu.

Katika utetezi wake, Sajenti Rogers alikiri kumpiga marehemu, akidai kuwa kijana huyo alikuwa akimjibu kwa dharau wakati wa mahojiano.

Baada ya kusikiliza jumla ya mashahidi sita wa upande wa Jamhuri na watatu wa upande wa utetezi, mahakama ilimtia hatiani mshtakiwa kwa kosa la kuua bila kukusudia, kinyume na vifungu vya 195 na 198 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, na kumhukumu kifungo cha miaka miwili jela.

Hata hivyo, baba mzazi wa marehemu, Nashon Kiyeyeu, ameonyesha kutoridhishwa na hukumu hiyo, akidai kuwa kitendo hicho kilifanywa kwa makusudi.

Ameiomba serikali pamoja na wadau wa haki kuingilia kati ili kuhakikisha haki inatendeka kikamilifu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here