BoT yahimiza matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali kuimarisha biashara EAC

DAR-Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bi. Sauda Msemo amesisitiza umuhimu wa kuharakisha matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali katika biashara za mipakani ili kuongeza ufanisi, kupunguza gharama na kukuza ujumuishwaji wa kifedha nchini na ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Uwezeshaji wa Malipo ya Kidijitali kwa Wafanyabiashara wa Mipakani uliofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 31 Machi 2026, Bi. Msemo amesema kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana katika upanuzi wa huduma za kifedha za kidijitali, bado biashara nyingi za mipakani zinafanyika kwa kutumia fedha taslimu.
Amesema utegemezi huo wa fedha taslimu unasababisha changamoto mbalimbali za kimuundo, ikiwemo gharama kubwa za miamala, hatari za kiusalama, ukosefu wa uwazi pamoja na kuwanyima wafanyabiashara, hususan wanawake na vijana, fursa ya kupata huduma rasmi za kifedha.
Bi. Msemo alibainisha kuwa taarifa zilizokusanywa kutoka katika maeneo ya mipakani kama Namanga, Mutukula na Rusumo, pamoja na vituo vikuu vya biashara vya Arusha, Bukoba na Mwanza, zinaonesha wazi haja ya kuchukua hatua madhubuti na shirikishi ili kuondoa vikwazo vinavyokwamisha matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali.
Alieleza kuwa mdahalo huo ni fursa muhimu ya kujadili na kukubaliana juu ya vipaumbele na suluhisho zitakazochochea matumizi ya mifumo salama, nafuu na jumuishi ya malipo ya kidijitali katika biashara za mipakani.
“Lengo letu la pamoja ni kujenga mfumo wa malipo unaoweza kuunganika, unaopatikana kwa urahisi, wenye gharama nafuu na unaoaminika, ili kuwezesha miamala ya mipakani kufanyika kwa urahisi na kuchochea ushirikiano wa kiuchumi kikanda,” amesema.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za umma, wadau wa sekta ya fedha, watoa huduma za kifedha na wabunifu wa teknolojia katika kufanikisha azma hiyo, huku akibainisha kuwa ni muhimu pia kuhakikisha suluhisho zinazopatikana zinazingatia mahitaji halisi ya wafanyabiashara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here