NA LWAGA MWAMBANDE
MACHI 30,2026 Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imepongezwa kwa usimamizi madhubuti wa sekta ya kibenki unaochangia kuimarika kwa faida za mabenki na ustawi wa sekta ya fedha nchini Tanzania.
Pongezi hizo zimetolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa NCBA Group, Bw.John Gachora, wakati wa ziara yake katika Benki Kuu ya Tanzania alipokutana na kufanya mazungumzo na Gavana wa benki hiyo, Bw. Emmanuel Tutuba jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo, pande hizo mbili zilijadili masuala mbalimbali ya kimkakati, ikiwa ni pamoja na dhamira ya Nedbank Group Limited ya kununua asilimia 66 ya hisa za NCBA Group Limited, hatua inayotarajiwa kuwa na mchango katika kuimarisha ushirikiano wa kifedha ndani ya kanda.
Bw. Gachora alibainisha kuwa,ukuaji wa faida za mabenki unatokana na usimamizi thabiti wa BoT pamoja na uwepo wa mazingira wezeshi kwa taasisi za kifedha kufanya shughuli zake kwa ufanisi nchini Tanzania.
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anabainisha kuwa,pongezi hizo kwa Benki Kuu ya Tanzania zinaashiria mambo manne muhimu katika muktadha wa sekta ya fedha nchini.
Mosi, zinaonesha kuwa,kuna imani ya juu kutoka kwa wadau wa kimataifa wakiwemo viongozi wa taasisi kama NCBA Group juu ya uimara wa usimamizi wa sekta ya kibenki nchini.
Pili, ni ishara ya uthabiti wa mfumo wa fedha, ambapo mabenki yanafanya kazi katika mazingira salama, yanayotabirika na yenye kanuni zinazosimamiwa ipasavyo.
Tatu, zinaashiria kuwa sera na mifumo inayosimamiwa na BoT inachochea ukuaji wa biashara za kibenki, jambo linaloonekana kupitia ongezeko la faida za mabenki.
Nne, pongezi hizi pia zinaongeza mvuto kwa wawekezaji wa ndani na nje, kwani zinajenga taswira chanya ya Tanzania kama eneo salama na lenye fursa katika uwekezaji wa sekta ya fedha.
Kwa ujumla, ni uthibitisho kuwa usimamizi wa BoT unachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo na ushindani wa sekta ya fedha nchini.Endelea,
1. Kwanza unajisifia, na watu kukusifia,
Vile unajisifia, mwenye wajiangalia,
Ila wakikusifia, hakika umetimia,
Benki Kuu kusifiwa, pongezi zifike kwenu.
2. Hao wanawasifia, wageni wametujia,
Vile wameangalia, kazi njema Tanzania,
Ile mnajifanyia, uchumi umetulia,
Benki Kuu kusifiwa, pongezi zifike kwenu.
3. Usimamizi thabiti, Benki Kuu Tanzania,
Sana mmejizatiti, sekta twaiangalia,
Benki zinakuwa fiti, faida inaingia,
Benki Kuu kusifiwa, pongezi zifike kwenu.
4. Kuna mchango mkubwa, mabenki kusimamia,
Vihatarishi vyazibwa, biashara yatulia,
Kisha faida kubwa, nchini inabakia,
Benki Kuu kusifiwa, pongezi zifike kwenu.
5. Ni mtendaji mkuu, benki Kenya asifia,
Jinsi vile Benki Kuu, sekta inasimamia,
Nami nafanya nukuu, hili kulishangilia,
Benki Kuu kusifiwa, pongezi zifike kwenu.
6. Na ustawi wa benki, hapa kwetu Tanzania,
Huo unayo mantiki, hata unatufikia,
Benki Kuu yabariki, jinsi inasimamia,
Benki Kuu kusifiwa, pongezi zifike kwenu.
7. Benki sasa ziko nyingi, watu zawahudumia,
Kazi kwao ya msingi, mitaji kutupatia,
Hapo zaupiga mwingi, vema tukawasifia,
Benki Kuu kusifiwa, pongezi zifike kwenu.
8. Hapo kuna uongozi, Benki Kuu wachangia,
Sana unafanya kazi, sekta kusimamia,
Sasa matokeo wazi, wageni wanasifia,
Benki Kuu kusifiwa, pongezi zifike kwenu.
9. Na mazingira ya kwetu, kuwekeza yavutia,
Benki za nje za kwetu, hayo zinayatumia,
Kwa maendeleo yetu, pazuri tutafikia,
Benki Kuu kusifiwa, pongezi zifike kwenu.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
