NA DIRAMAKINI
KATIKA kuimarisha ubora na uaminifu wa elimu ya fedha kwa umma, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeweka msisitizo kwa waelimishaji waliothibitishwa kuzingatia maadili na miongozo ya programu, huku ikionya wachache wanaokiuka miongozo kwani watachukuliwa hatua kali.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Machi 31,2026 na Gavana wa BoT, Bw.Emmanuel Tutuba.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Baraza la Taifa la Huduma Jumuishi za Kifedha pamoja na wadau wa sekta ya fedha, ilizindua Mtaala wa Waelimishaji Waliothibitishwa wa Elimu ya Fedha (Certified Financial Educators-CFE) Desemba 2023, kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya uelewa mdogo wa masuala ya kifedha miongoni mwa wananchi walio nje ya mfumo rasmi wa elimu.
Programu hiyo inatekelezwa kupitia Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Benki Kuu ya Tanzania na taasisi za elimu, mafunzo na utaalamu zilizoidhinishwa, ikiwa na lengo la kuleta uratibu katika utoaji wa elimu ya fedha, kuongeza ufanisi na kuimarisha ubora wa huduma hiyo nchini kupitia matumizi ya majukwaa ya kitaaluma.
Aidha,tangu kuanza kwa utekelezaji wake, zaidi ya watu 1,388 wamethibitishwa na kwa sasa wanatoa elimu ya fedha kwa umma kupitia mbinu mbalimbali zikiwemo semina, mikutano na mitandao ya kijamii.
"Tathmini ya awali inaonesha kuwepo kwa mabadiliko chanya katika tabia za kifedha, hususan katika matumizi ya bidhaa na huduma za akiba na uwekezaji.
"Hata hivyo, kumebainika changamoto ya baadhi ya waelimishaji kutoa taarifa zisizo sahihi au kuwasilisha ujumbe usioendana na malengo ya programu."
Kufuatia hali hiyo, Benki Kuu imewakumbusha waelimishaji hao kuzingatia maadili na miongozo ya programu, ikiwemo kufundisha maudhui yaliyoidhinishwa, kutumia utambulisho rasmi wa programu na kuepuka kuwasilisha vibaya hadhi ya cheti hicho.
Aidha, imeelezwa kuwa cheti cha Waelimishaji Waliothibitishwa wa Elimu ya Fedha hakimpi mhusika hadhi ya kuwa taasisi ya fedha, mfanyakazi wa Benki Kuu, dalali wa masoko ya fedha, kocha au mshauri wa kifedha.
Waelimishaji wanapaswa pia kuendelea kuzingatia viwango vya taaluma vinavyotambuliwa na taasisi husika.
Benki Kuu imesisitiza kuwa, haitasita kuchukua hatua stahiki, ikiwemo kufuta vyeti, kwa waelimishaji watakaokiuka masharti ya programu.
Wakati huo huo, BoT imeendelea kutambua mchango wa waelimishaji hao katika kuelimisha umma na kuwahimiza kuendeleza taaluma, uadilifu na uzingatiaji wa viwango vilivyowekwa.

