DAR-Katibu Mkuu Wizara ya Fedha,Dkt.Natu El-maamry Mwamba ametembelewa na watendaji wa Sekretarieti ya Kikundi cha Kudhibiti Fedha Haramu cha Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (ESAAMLG) wakiongozwa na Katibu Mtendaji wa Sekretarieti hiyo, Bi.Fikile Zitha. 

Pamoja na mambo mengine yaliyojadiliwa, lengo kubwa la ziara hiyo ilikuwa ni kuendeleza ushirikiano wa kiutendaji kati ya taasisi hiyo na nchi ya Tanzania na kuangalia namna ya kuisaida Tanzania kiutalaam katika hatua inayofuata ya kazi ya tathimini ya nchi ya Tanzania kuhusu mifumo ya udhibiti wa fedha haramu inayotarajiwa kufanyika mwaka 2028.
Katika mkutano huo Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, aliishukuru Sekretarieti ya ESAAMLG kwa namna inavyoshirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali ya udhibiti wa fedha haramu, hususani katika kutoa ushauri wa kitaalam uliosababisha Tanzania kuondolewa katika orodha ya nchi zenye mifumo dhaifu ya Udhibiti wa Fedha Haramu duniani.
Kwa upande wa Sekretareti ya ESAAMLG, Katibu Mtendaji wa Sekreatariat hiyo Bi. Fikile Zitha, aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuwa mwenyeji wa umoja huo wenye nchi 22 sasa, pia kwa kuipatia ESAAMLG majengo mapya ya Ofisi ya taasisi hiyo ambapo jengo moja limekwishaanza kutumika na jingine bado lipo katika hatua za mwisho za maboresho.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Naibu Gavana ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kudhibiti Fedha Haramu, Bi. Sauda Msemo, Kamishna wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kudhiniti Fedha Haramu, Bw. Majaba Magana, Kamishna Msaidizi wa Idara ya Fedha za Nje Wizara ya Fedha, Bw. James Msina na wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Fedha na Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu.





