NA DIRAMAKINI
JESHI la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi limetangaza mikakati kabambe ya kuimarisha ulinzi na usalama kwa wananchi katika kipindi hiki cha kuelekea maadhimisho ya Eid el-Fitri, likisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa jamii katika kudumisha amani na utulivu.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo,SACP Richard Mchomvu imeeleza kuwa, hatua madhubuti zimeandaliwa kuhakikisha usalama unaimarishwa katika maeneo yote muhimu, ikiwemo sehemu za ibada, viwanja vya mikusanyiko ya watu pamoja na maeneo ya kijamii yatakayokuwa na msongamano mkubwa wa wananchi wakati wa sikukuu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi,SACP Richard Thadei Mchomvu.
Katika kuimarisha operesheni hizo, Jeshi la Polisi limepanga kuongeza doria na misako ya mara kwa mara zitakazohusisha askari wa miguu, magari, pikipiki na vikosi maalum, ikiwemo kikosi cha mbwa na farasi.
Hatua hiyo inalenga kudhibiti na kuzuia vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha amani ya wananchi.
Wananchi wamehimizwa kuchukua tahadhari binafsi wanaposherehekea sikukuu hiyo, ikiwa ni pamoja na kulinda mali zao wanapokuwa mbali na makazi yao, pamoja na kufuatilia mienendo ya watoto ili kuepuka matukio ya kihalifu yanayoweza kujitokeza.
Katika kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara, Jeshi la Polisi limetangaza kufungwa kwa muda kwa baadhi ya barabara muhimu, zikiwemo barabara zinazoelekea eneo la Kariakoo, Maisara hadi Mnazi Mmoja, pamoja na Baraza la Wawakilishi la zamani hadi Magazeti, miongoni mwa nyingine.
Aidha, askari wa usalama barabarani wataongezwa kwa wingi ili kusimamia nidhamu ya madereva na kuhakikisha sheria za usalama barabarani zinafuatwa kikamilifu.
Madereva wote wametakiwa kuendesha kwa tahadhari, kuwa na leseni halali na kuhakikisha vyombo vyao vipo katika hali nzuri kiusalama.
Onyo Dhidi ya Uhalifu na Utapeli
Sambamba na maandalizi hayo, Jeshi la Polisi limetoa tahadhari kuhusu kuongezeka kwa viashiria vya uhalifu, likitolea mfano tukio la hivi karibuni ambapo baadhi ya waendesha pikipiki waliwashambulia maafisa wa mamlaka ya usafirishaji waliokuwa wakitekeleza majukumu yao katika eneo la Darajabovu.
Tukio hilo limeelezwa kuwa ni kinyume cha sheria na linachukuliwa hatua kali dhidi ya wahusika.
Aidha, Jeshi la Polisi limeonya juu ya ongezeko la matukio ya uhalifu wa kimtandao, ambapo wahalifu hutumia mbinu mbalimbali za utapeli.
Baadhi yao hujifanya mawakala wa huduma za simu wakitumia vitambulisho bandia ili kuwaaminisha wananchi na hatimaye kuwaibia fedha, hususan kupitia huduma za kifedha za simu.
Mbinu nyingine zinazotajwa ni pamoja na kupiga simu za udanganyifu wakijifanya wanatoa ajira au huduma mbalimbali na kuwaomba wananchi fedha, pamoja na wizi wa simu unaotumiwa baadaye kuwatapeli ndugu na marafiki wa mhusika kupitia mawasiliano yaliyopo kwenye simu hizo.
Kutokana na hali hiyo, wananchi wametakiwa kuwa makini kwa kutotoa taarifa zao binafsi kwa watu wasiowafahamu, na kutoa taarifa kwa vyombo vya dola mara wanapobaini viashiria vya uhalifu.
Pia, wametakiwa kuripoti mara moja wanapopoteza simu zao ili kuzuia matumizi mabaya ya taarifa.
Vilevile, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi limetoa wito kwa wananchi kusherehekea sikukuu ya Eid el-Fitri kwa amani, utulivu na kuzingatia sheria za nchi, likisisitiza kuwa sikukuu isiwe chanzo cha vitendo vya uhalifu kama vile wizi, uporaji, unyang’anyi au udhalilishaji.
Aidha, onyo kali limetolewa kwa yeyote atakayejihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani au kujipatia kipato kwa njia zisizo halali, kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake bila kusita.
Jeshi la Polisi limemalizia kwa kuwatakia wananchi wote sikukuu njema na salama ya Eid el-Fitri.
