MOROGORO-Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) amesema kuwa,Serikali itaendelea kufanyia kazi maombi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima ya kutafuta suluhisho la kudumu la kutatua changamoto ya mafuriko yanayoikabili mkoa huo mara kwa mara nyakati za masika na kuathiri maisha ya wananchi.
Mhe. Balozi Omar amesema hayo mjini Morogoro alipofanya ziara ya kujitambulisha katika Ofisi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Morogoro, ambapo alilakiwa na Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo, Comrade Mhandisi Joseph Masunga.
Alisema kuwa, hatua hizo ni pamoja na kujenga miundombinu ya kudhibiti mafuriko haho ikiwemo ujenzi wa mabwawa ya maji yatakayotumika katika shughuli nyingine za uzalishani kama vile kilimo cha umwagiliaji na kuhudumia mifugo wakati wa kiangazi.Aidha, Mhe.Balozi Omar alisema kuwa ujio wake katika Ofisi za CCM Mkoa kujitambulisha kama Waziri wa Fedha na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa (NEC), ni utaratibu aliojiwekea kwani anatambua Chama kilichoshika madaraka ndicho chenye wajibu wa kuisimamia Serikali ili kuhakikisha ilani ya Chama inatekelezwa ipasavyo kuwahudumia na kuwaletea wananchi maendeleo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Morogoro, Comrade Mhandisi Joseph Masunga, alimpongeza Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), kwa kutambua umuhimu wa Chama katika kuisimamia Serikali na kwamba ni Waziri pekee aliyepanga ziara ya kutembelea na kujitambulisha katika Ofisi za Chama akiwa katika majukumu yake ya kikazi mkoani humo tangu Mwenyekiti huyo ashike nafasi hiyo.
Aidha, Comrade Masunga alisema Chama cha Mapinduzi mkoani humo kinaendelea na kuisimamia Serikali katika kutekeleza Ilani ya Chama pamoja na kuendelea na ukarabati wa miundombonu ya jengo la CCM mkoani humo na kuomba wadau mbalimbali kuchangia ukarabati huo.

