DODOMA-Wizara ya Fedha kupitia Idara ya Usimamizi wa Bajeti ya Serikali, inaendelea na uchambuzi wa bajeti ya sekta ya uzalishaji kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Sekta hiyo inajumuisha Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Ardhi, Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Wizara ya Madini.
Hatua hiyo inalenga kuchambua na kujadili mipango na mapendekezo ya bajeti ya sekta muhimu za uzalishaji ili kuhakikisha yanazingatia vipaumbele vya Taifa, sera za maendeleo, mikakati ya kitaifa pamoja na miongozo ya upangaji na uandaaji wa bajeti.
Kikao hicho kimeongozwa na Kamishna Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Bajeti ya Serikali, Bw. Fundi Makama na kuhudhuriwa na Wakurugenzi wa Sera na Mipango pamoja na wataalamu kutoka wizara na sekta husika.Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma ambapo, washiriki walipata nafasi ya kujadili kwa kina namna bajeti za sekta za uzalishaji zinavyoweza kuyafikia malengo yaliyowekwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kuimarisha uchumi wa Taifa na kuchochea maendeleo endelevu.



