■Marekebisho yahusisha mabasi ya masafa marefu, daladala, teksi mtandao na pikipiki mtandao
NA DIRAMAKINI
MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetangaza rasmi viwango vipya vya nauli kwa huduma mbalimbali za usafiri nchini, ikiwa ni sehemu ya maboresho ya udhibiti wa sekta hiyo.
Marekebisho hayo yanahusisha mabasi ya masafa marefu, mabasi ya mijini (daladala), pamoja na huduma za teksi mtandao na pikipiki mtandao.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo, uamuzi huo umefanyika kwa kuzingatia kifungu cha 19 cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, Sura ya 413, kinachoiruhusu LATRA kupanga na kurekebisha viwango vya nauli na tozo za huduma za usafiri ili kulinda maslahi ya wadau wote, wakiwemo watumiaji na watoa huduma.
Katika viwango vipya vilivyotolewa, nauli za mabasi ya masafa marefu zimeainishwa kulingana na daraja la basi pamoja na hali ya barabara.
Kwa mabasi ya kawaida (ordinary), abiria atalipa Sh57.93 kwa kila kilometa moja katika barabara za lami, huku kwa barabara za vumbi nauli ikiwa Sh66.62 kwa kilometa.
Kwa upande wa mabasi ya daraja la kati (semi-luxury), nauli imepangwa kuwa Sh74.18 kwa kila kilometa moja katika barabara za lami, hatua inayolenga kuendana na ubora wa huduma zinazotolewa katika daraja hilo.
Aidha, LATRA imefanya marekebisho ya nauli kwa mabasi ya mijini (daladala), ambapo safari ya umbali wa hadi kilometa 10 sasa itagharimu Sh700.
Nauli hiyo itaongezeka kulingana na umbali wa safari, na kufikia kiwango cha juu cha Sh1,500 kwa safari ya kati ya kilometa 36 hadi 40.
Tangazo hilo limetolewa kupitia Gazeti la Serikali, na viwango hivyo vipya vinatarajiwa kuanza kutumika rasmi siku 14 baada ya kutangazwa kwake, kwa mujibu wa taratibu za kisheria.
Marekebisho haya yanatarajiwa kuwa na athari kwa wadau mbalimbali wa sekta ya usafiri, hususan katika kuimarisha uwiano kati ya gharama za uendeshaji na uwezo wa wananchi kumudu huduma za usafiri.
Tags
Breaking News
Habari
LATRA Tanzania
LATRA yatangaza nauli mpya
NAULI MPYA
Nauli za Daladala
Viwango vya Nauli
