DODOMA-Tanzania ni taifa lisilofungamana na upande wowote na limejikita katika kulinda mamlaka ya nchi, mipaka yake pamoja na uhuru wa kisiasa.
Hayo yamesemwa na Mbunge wa Singida Magharibi, Mhe.Elibariki Kingu, bungeni jijini Dodoma alipochangia Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iliyowasilishwa bungeni hapo Mei 26, 2026.
Mhe. Kingu amesema Tanzania itaendelea kusimamia diplomasia yenye manufaa kwa pande zote kwa kuweka kipaumbele katika kuvutia uwekezaji, kukuza biashara na kupata masoko ya bidhaa za Tanzania kimataifa.
“Hatuchukii wageni wala kuchukiana sisi kwa sisi. Sisi ni kaka na dada. Tunaoleana na kuishi pamoja, Tanzania ni mfano wa kuigwa Afrika kwa namna ilivyoweza kuishi kwa amani katika jamii na familia zenye imani tofauti za kidini bila migogoro,” alisema Kingu.
Aidha, alisisitiza kuwa Tanzania inathamini uhusiano wake na mataifa yote duniani na iko tayari kushirikiana na taifa lolote kwa misingi ya kuheshimiana na manufaa ya pamoja.
Akihitimisha mchango wake, Mhe. Kingu alitoa wito wa kujengwa kwa mfumo wa kimataifa wenye amani, usio na uonevu, ubabe wala unyonyaji dhidi ya mataifa madogo.
“Kila taifa, bila kujali ukubwa wake au nguvu zake kiuchumi, linastahili heshima, utu na mamlaka kamili ya kujitawala,”alisisitiza.

