ARUSHA-Mawakili wa Serikali wamehimizwa na kusisitizwa kuendelea kusimamia mashauri ya Serikali na kuitetea Serikali kwa ujumla katika vyombo vya ndani na nje ya nchi.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba akiwasili kwa ajili ya kufunga mafunzo kwa Mawakili wa Serikali yaliyofanyika jijini Arusha.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba (Mb), wakati akifunga mafunzo kwa Mawakili wa Serikali wa kutoka Wizara mbalimbali, taasisi za Serikali, Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ambayo yamefanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia tarehe 18 hadi 22 Mei, 2026 jijini Arusha.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba akizungumza na Mawakili wa Serikali wakati akifunga mafunzo kwa Mawakili hao yaliyofanyika jijini Arusha.
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt.Ally Possi akizungumza na Mawakili wa Serikali wakati wa kufunga mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Arusha.
Mhe. Katimba amesema kuwa Serikali inawategemea sana Mawakili wa Serikali katika kulinda rasilimali za Taifa kupitia ushauri wa kisheria wenye tija na usimamizi madhubuti wa mashauri mbalimbali.
“Hivyo, baada ya mafunzo haya tunatarajia muweze kusimamia kwa ufanisi mashauri ya Serikali; kuimarisha usimamizi wa mikataba na manunuzi ya umma; kushauri vizuri Serikali kuhusu sheria za kodi, anga na uwekezaji; kusimamia kwa weledi usuluhishi wa migogoro; na kuitetea Serikali kwa ufanisi katika vyombo vya ndani na kimataifa,” amesema Mhe. Katimba.
Pia, ameongeza kuwa mafunzo hayo yamekuja wakati muhimu ambapo Taifa linaelekea katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi wa kati unaojumuisha wananchi wote.
Ili kufikia malengo hayo, ni muhimu kuwa na taasisi imara za kisheria pamoja na wataalamu wenye uwezo wa kusimamia sheria, mikataba, uwekezaji, kodi na utatuzi wa migogoro kwa haki, uwazi na uwajibikaji.
“Kupitia ujuzi mlioupata, nina imani kuwa mtakuwa sehemu muhimu katika kuhakikisha kuwa sheria na mifumo ya Serikali inasimamiwa kwa weledi na kwamba matunda ya maendeleo yanawanufaisha wananchi wote kupitia mazingira bora ya uwekezaji, biashara na utoaji wa huduma za umma,” amesisitiza Mhe. Katimba.
Mwandishi Mkuu wa Sheria, ndugu Onorius Njole akitoa mada kuhusu Uandishi wa Sheria kwa Ufasaha na Kuzuia Migogoro wakati wa mafunzo kwa Mawakili wa Serikali yaliyofanyika jijini Arusha.
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice Mtulo akimsikiliza Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba (hayupo pichani) wakati akifunga mafunzo kwa Mawakili wa Serikali yaliyofanyika jijini Arusha.
Baadhi ya Mawakili wa Serikali wakimsikiliza Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba wakati akifunga mafunzo kwa Mawakili hao yaliyofanyika jijini Arusha.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Said Kalunde akitoa mada kuhusu kuelewa namna bora ya kuwahoji mashahidi katika usuluhishi wakati wa mafunzo kwa Mawakili wa Serikali yaliyofanyika jijini Arusha.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba akikabidhi tuzo kwa baadhi ya wadhamini wa mafunzo kwa Mawakili wa Serikali yaliyofanyika jijini Arusha. Anayeshuhudia kushoto ni Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba (aliyeketi katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Wakuu wa Vitengo vya Sheria wa Wizara na taasisi mbali mbali za Serikali baada ya kufunga mafunzo kwa Mawakili wa Serikali yaliyofanyika jijini Arusha.
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi amemueleza Mhe. Katimba kuwa, Mawakili hao wamepatiwa mafunzo na wakufunzi wabobezi wa taaluma mbalimbali ambapo mada mbalimbali zimetolewa zinazohusu dhamana za kibenki, usuluhishi wa ndani na nje ya nchi, usimamizi wa mikataba, sheria za kodi, sheria za anga pamoja na namna ya kuitetea Serikali katika mabaraza ya kimataifa ya uwekezaji.
“Mada hizi ni muhimu sana katika kuhakikisha Serikali inalindwa dhidi ya hasara na migogoro inayoweza kuzuilika kwa kuwa Mawakili wa Serikali sio tu Mawakili ila ni walinzi wa kalamu wanaolinda uchumi na rasilimali za taifa,” amesema Dkt. Ally Possi.
Pia, Dkt. Possi ameongeza kuwa Mawakili wa Serikali watazingatia mabadiliko ya nchi yetu yanayotarajiwa kutokea katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2050 na mwenendo wa dunia katika masuala mbalimbali.
Mafunzo haya yamefanyika kwa mara ya saba mfululizo ambapo yamekuwa yanafanyika mara moja kwa mwaka na yanaratibiwa na kuandaliwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.










