FREETOWN-Tanzania imesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa Kikanda katika kuongeza thamani Madini ya Almasi, uwazi katika usimamizi wa rasilimali madini na kuimarisha mchango wa Sekta ya Madini katika maendeleo ya uchumi wa nchi wanachama Zinazozalisha Madini ya Almasi Afrika (ADPA).
Hayo yalibainishwa Mei 19, 2026 mjini Freetown, Sierra Leone, na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo, ambaye anaongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki katika Mkutano wa 11 wa Kawaida wa Kamati ya Wataalam wa umoja huo.
Mkutano huo unawakutanisha wataalam kutoka nchi wanachama wa ADPA kujadili masuala mbalimbali yanayolenga kuimarisha usimamizi, biashara na maendeleo ya sekta ya almasi barani Afrika.Aidha, katika mkutano huo, wajumbe walijadili taarifa ya mwaka ya Mkurugenzi Mtendaji wa ADPA ya mwaka 2025, utekelezaji wa bajeti na taarifa za fedha za mwaka 2025 pamoja na taarifa ya ukaguzi wa nje wa hesabu kwa kipindi cha 2023–2024.
Aidha, masuala ya msamaha wa madeni, daftari la hatari, maendeleo ya uwezo wa taasisi na uanachama wa ADPA katika Shirika la Viwango Duniani (ISO) yalipata nafasi ya kujadiliwa kwa lengo la kuimarisha ufanisi wa taasisi hiyo.


