GEITA-Mkurugenzi na mmiliki wa Kadama English Medium Pre and Primary School,Leticia Pastory amewataka wanawake nchini kuendelea kupambana kudumisha malezi bora na ya asili kwa watoto ili kujenga kizazi chenye maadili na nidhamu.
Mkurugenzi wa Kadama English Medium Primary School, Leticia Pastory akiwa na tuzo ya kuwa mshindi wa kwanza kitaifa mwaka 2018 matokeo ya darasa la saba.
Leticia amesema hayo kuelekea tamasha la Geita Women Festival 2026 linalotarajiwa kufanyika mkoani Geita ambalo limeandaliwa na shirika la Geita Women and Youth Foundation.
Pastory ni mmoja wa wadhamini wa tuzo za wanawake wa dhahabu zitakazotolewa katika tamasha hilo Juni 6,2026.
Mkurugenzi wa Geita Women and Youth Foundation,Cecylia Miraji muandaaji wa tamasha la tuzo za mwanamke wa Dhahabu 2026.Mbali na kuwa mdhamini Leticia pia anawania tuzo ya Mkurugenzi Bora (CEO Bora) anayemiliki shule binafsi kutokana na mchango wake katika sekta ya elimu kupitia shule ya Kadama English Medium iliyopo Kata ya Buseresere Wilaya ya Chato karibu na Katoro.
Akizungumza kuhusu tamasha hilo, amesema wanawake wanapaswa kutumia fursa hiyo kupata elimu kutoka kwa wakufunzi mbalimbali watakaoshiriki kutoa mada za maendeleo,malezi na ujasiriamali.
“Wanawake wana nafasi kubwa katika malezi ya watoto na ustawi wa jamii. Ni muhimu kuendelea kulinda maadili ya familia na kuhakikisha watoto wanapata malezi bora yenye msingi wa utamaduni wetu,” amesema Leticia.
Katika kipindi cha miaka 17 tangu kuanzishwa kwa shule hiyo ya Kadama English Medium primary imefanikiwa kupata jumla ya tuzo saba kutokana na matokeo bora ya kitaaluma.
Shule hiyo pia imewahi kuandika historia kwa kutoa mwanafunzi wa kwanza kitaifa na mwanafunzi wa kumi kitaifa katika matokeo ya darasa la saba.
Leticia Pastory ambaye ni Mkurugenzi wa Kadama English Medium Primary School akiwa na baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo.Iwapo Leticia atafanikiwa kushinda tuzo ya CEO Bora mwaka 2026 itakuwa ni tuzo ya nane kwa shule hiyo ambayo imeendelea kuwa miongoni mwa shule zinazofanya vizuri kitaifa.




