Tanzania ina fursa kubwa ya kufikia Dira ya Maendeleo 2050, yasema IMF huku ikitarajiwa kutoa dola milioni 375.5 nchini

DAR-Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Serikali ya Tanzania zimefikia makubaliano ya ngazi ya wataalamu kuhusu kukamilika kwa tathmini za mwisho za programu za Mfuko wa Mikopo Nafuu (ECF) na Mfuko wa Ustahimilivu na Uendelevu (RSF).
Hatua hii itawezesha Tanzania kupata ufadhili wa takribani dola za Marekani milioni 375.5 baada ya kuidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi ya IMF.

Fedha hizo zitachangia jumla ya msaada wa dola bilioni 1.052 kupitia ECF kwa ajili ya kuimarisha uchumi na sekta za uzalishaji na huduma za jamii, pamoja na dola milioni 563.8 kupitia RSF kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi tangu kuanza kwa programu hizo.
Taarifa hiyo imetolewa na IMF kupitia Kiongozi wa Timu yake ya Wataalamu, Nicolas Blancher, kufuatia kikao cha kuhitimisha ziara ya timu hiyo kilichofanyika tarehe 12 Mei 2026 katika Benki Kuu ya Tanzania, jijini Dar es Salaam.

Katika kikao hicho, upande wa Tanzania uliongozwa na Waziri wa Fedha, Khamis Mussa Omar (Mb), na pia kilihudhuriwa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba.

Bw. Blancher alisema IMF imeridhishwa na utekelezaji wa programu hizo, akibainisha kuwa malengo makuu ya kiuchumi yamefikiwa kwa kiwango kikubwa.
Alieleza kuwa uchumi umeendelea kukua kwa kasi, mfumuko wa bei umebaki ndani ya lengo la Benki Kuu ya Tanzania, na akiba ya fedha za kigeni iko katika kiwango cha kuridhisha.

Aidha, alibainisha kuwa matumizi ya Serikali katika sekta za elimu na afya yameongezeka, sambamba na hatua za kuimarisha ustahimilivu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi. Uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua kwa asilimia 5.9 mwaka 2026 huku mfumuko wa bei ukibaki kati ya asilimia 3 hadi 5.
Kwa mtazamo wa muda wa kati na mrefu, IMF imeeleza kuwa Tanzania ina nafasi nzuri ya kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo 2050 iwapo itaendeleza mageuzi ya kukuza rasilimali watu, kuboresha mazingira ya biashara, kuimarisha usimamizi wa fedha za umma na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, alihakikisha kuwa Serikali itaendelea kutekeleza programu hizo kwa umakini ili kuhakikisha uchumi unaendelea kuwa imara, jumuishi na wenye tija kwa maendeleo ya taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here