Watumishi wa Umma wataendelea kunufaika na maboresho ya Serikali-Waziri Ridhiwani Kikwete

ARUSHA-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete amesema,Serikali itaendelea kuboresha mazingira na maslahi ya watumishi wa umma nchini kadri hali ya bajeti itakavyoruhusu, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya kuimarisha ustawi wa wafanyakazi wa sekta ya umma.
Waziri Kikwete ameyasema hayo leo wakati akishiriki ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 13 wa Chama cha Waandishi Waendesha Ofisi Tanzania (TAPSEA) uliofanyika katika eneo la Ngurdoto mkoani Arusha.

Mkutano huo umefunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Emanuel Nchimbi na kuwahusisha wajumbe wapatao 5,050 kutoka taasisi mbalimbali za Serikali, halmashauri pamoja na taasisi za umma kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Akizungumza katika mkutano huo, Dkt. Nchimbi amewataka wanachama wa TAPSEA kuhakikisha wanazingatia haki, uwazi na mshikamano katika uchaguzi wa viongozi wapya wa chama hicho, huku akionya dhidi ya vitendo vinavyoweza kuathiri mwelekeo na misingi ya umoja huo wa kitaaluma.

Waziri Ridhiwani Kikwete amesema,Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha ustawi wa watumishi wa umma nchini.
Ameeleza kuwa,hatua hizo ni pamoja na upandishaji wa madaraja kwa watumishi, maboresho ya miundo na vyeo vya kazi, pamoja na ulipaji wa madeni ya mishahara na stahiki mbalimbali ambazo zilikuwa zikisubiriwa kwa muda mrefu.

Aidha, amesema Serikali imejipanga kuendelea kutekeleza maboresho hayo katika mwaka mpya wa bajeti na katika vipindi vijavyo kulingana na upatikanaji wa fedha.
“Tumeendelea kuhakikisha watumishi wanapata haki zao kwa wakati, ikiwa ni pamoja na kupandishwa madaraja,kuboreshwa kwa miundo ya kazi na kulipwa madeni mbalimbali ya mishahara. Serikali itaendelea kufanya hivyo kila pale bajeti itakapopatikana,” amesema Waziri Kikwete.
Mkutano huo wa TAPSEA unatarajiwa kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya taaluma ya uandishi na uendeshaji wa ofisi pamoja na kufanya uchaguzi wa viongozi wapya watakaoongoza chama hicho kwa kipindi kijacho.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here