NA DIRAMAKINI
JUMLA ya baiskeli 337 zimetolewa kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii katika Manispaa ya Songea na Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, hatua inayolenga kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi hususan katika maeneo ya vijijini na maeneo yenye changamoto za usafiri.
Baiskeli hizo zimetolewa kwa ufadhili wa kampuni ya Buffalo Bicycles Tanzania Limited, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuunga mkono Serikali katika kuboresha huduma za afya ya msingi na kuwawezesha wahudumu wa afya kuwafikia wananchi kwa urahisi zaidi.
Manispaa ya Songea imepokea baiskeli 140 zilizogawiwa katika vituo mbalimbali vya afya ambapo Kituo cha Afya Mjimwema kimepata baiskeli 49, Kituo cha Afya Msamala baiskeli 27 na Kituo cha Afya Ruvuma baiskeli 64.
Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Songea imekabidhiwa baiskeli 197, zikiwemo 100 zilizotolewa kwa Zahanati ya Peramiho, 58 kwa Kituo cha Afya Magagula na 39 kwa Hospitali ya Mpitimbi.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Peres Magiri amesema,wahudumu wa afya ngazi ya jamii ni mhimili muhimu katika utoaji wa huduma za tiba kinga na kiungo muhimu kati ya jamii na mfumo rasmi wa huduma za afya.
Amesema,wahudumu hao wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kutoa elimu ya afya, kufuatilia huduma za chanjo, lishe, afya ya uzazi na maendeleo ya mtoto, hivyo upatikanaji wa usafiri utawawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
“Wahudumu wa afya ngazi ya jamii ni daraja muhimu linalounganisha kaya na miundombinu ya afya. Kupatikana kwa baiskeli hizi kutarahisisha utoaji wa elimu ya afya ya msingi, ufuatiliaji wa chanjo, lishe na huduma za afya ya uzazi, jambo ambalo lina mchango mkubwa katika kuokoa maisha ya wananchi kwa kuwahamasisha kupata huduma za afya mapema,”amesema Magiri.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Louis Chomboko amesema,msaada huo utasaidia kuongeza ufanisi wa huduma za afya katika ngazi ya jamii kwa kupunguza changamoto za usafiri zinazowakabili wahudumu hao wakati wa kutekeleza majukumu yao.
Dkt. Chomboko amebainisha kuwa,maeneo mengi yanayohudumiwa na wahudumu wa afya yapo mbali na vituo vya kutolea huduma za afya, hivyo uwepo wa baiskeli hizo utaongeza kasi ya kuwafikia wananchi na kutoa huduma kwa wakati.
Naye Meya wa Manispaa ya Songea, Abraham Mbunda amewataka wahudumu wa afya ngazi ya jamii kutumia vyema vifaa hivyo na kuendelea kutoa huduma kwa weledi, uadilifu na lugha yenye staha wanapowasiliana na wananchi.
Amesema,mafanikio ya huduma za afya katika jamii yanategemea kwa kiasi kikubwa namna wahudumu wanavyojenga mahusiano mazuri na wananchi pamoja na kuwapa elimu sahihi kuhusu masuala mbalimbali ya afya.
Kwa upande mwingine, Meneja wa Mradi wa kampuni ya Buffalo Bicycles Tanzania Limited, Delfina Kubel amesema,kampuni hiyo imeendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha huduma za afya jumuishi kwa kuhakikisha wahudumu wa afya wanapata vitendea kazi vinavyorahisisha utekelezaji wa majukumu yao.
Amesema,lengo la kampuni hiyo ni kusaidia kuongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi, hususan wale wanaoishi katika maeneo ya mbali, kwa kuwawezesha wahudumu wa afya kuwafikia kwa haraka na kwa urahisi zaidi.
Ugawaji wa baiskeli hizo unatarajiwa kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za afya ngazi ya jamii, kuimarisha kampeni za kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali na kuchangia juhudi za Serikali za kuboresha afya na ustawi wa wananchi katika Mkoa wa Ruvuma.

