Kombe la Dunia 2026:England yaichapa Croatia mabao 4-2,makocha wacharuka kipindi cha mapumziko

NA DIRAMAKINI

TIMU ya Taifa ya England imeanza vyema kampeni yake ya Kombe la Dunia 2026,baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Croatia katika mchezo wa Kundi L uliochezwa jijini Dallas, Marekani.
Mabao ya England yamefungwa na Harry Kane dakika ya 12' (P) na kuongeza lingine dakika ya 42' huku Jude Victor William Bellingham akipiga chuma kingine dakika ya 47' na Marcus Rashford akazamisha bao la nne dakika ya 85'.

Aidha, Croatia iliandika bao lake la kwanza dakika ya 36' kupitia kwa Martin Baturina na Petar Musa akamalizia bao la pili dakika ya 45'.

Ushindi huo ulitokana na mabadiliko makubwa yaliyofanywa na kikosi cha England kutoka kwa kocha mkuu Thomas Tuchel na msaidizi wake Anthony Barry katika kipindi cha pili baada ya mapumziko.

Katika kipindi cha kwanza, England ilionekana kuyumba na kushindwa kuonesha ubora uliotarajiwa licha ya mshambuliaji nahodha Harry Kane kufunga mabao mawili.

Kila England ilipopata bao la kuongoza, Croatia ilijibu na kusawazisha, jambo lililofanya timu hizo kwenda mapumzikoni zikiwa sare.

Ripoti kutoka kambini mwa England zinaeleza kuwa,Anthony Barry aliwakosoa vikali wachezaji kwa kuonesha mchezo aliouelezea kuwa wa "kuchanganya na usioeleweka", huku Tuchel naye akitoa maelekezo makali na kuwataka wachezaji wake kuongeza kasi, nidhamu na umakini katika kipindi cha pili.

Maneno hayo yalionekana kuzaa matunda mara baada ya kurejea uwanjani, ambapo England ilionesha sura tofauti kabisa kwa kutawala mchezo na kufunga mabao mawili zaidi yaliyohitimisha ushindi wa mabao 4-2.

Harry Kane aliendelea kuthibitisha umuhimu wake katika kikosi hicho kwa kuwa mhimili wa ushambuliaji, huku ushindi huo ukiipa England mwanzo mzuri katika mbio za kufuzu hatua ya mtoano.

Kwa upande wa Croatia, licha ya kuonesha uwezo mkubwa wa kupambana katika kipindi cha kwanza, ilishindwa kuhimili presha ya England baada ya mapumziko na kujikuta ikianza mashindano hayo bila pointi.

Matokeo hayo yanaifanya England kujikusanyia pointi tatu muhimu katika Kundi L na kutuma ujumbe kwa wapinzani wake kuwa ni moja ya timu zinazowania kutwaa taji la Kombe la Dunia 2026.

Ushindi huo pia utamwongezea Tuchel kujiamini katika juhudi zake za kuiongoza England kutafuta mafanikio makubwa kwenye michuano hiyo, huku mashabiki wa Three Lions wakipata sababu ya kuamini kuwa kikosi chao kina uwezo wa kwenda mbali zaidi katika mashindano hayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here