NA MARY GWERA
Mahakama-Zanzibar
JAJI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa George Masaju leo Juni, 22,2026 amemtembelea Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi na kufanya naye mazungumzo mafupi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi (kulia) akizungumza na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju alipomtembelea Ikulu Zanzibar leo tarehe 22 Juni, 2026.Katika mazungumzo yao, Rais Mwinyi amempongeza Jaji Mkuu kwa kushika wadhifa huo na kupongeza ushirikiano uliopo baina ya Mahakama ya Zanzibar na Mahakama ya Tanzania na kusisitiza juu ya umuhimu wa kuuendeleza ili kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Mahakama kwa manufaa ya wananchi.
“Nami nichukue kwanza fursa hii kukupa pongezi ya kuwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hongera sana na tunataka kukuhakikishia ushirikiano wetu, bahati nzuri tayari tuna ushirikiano mzuri sana kati ya Majaji Wakuu wa pande mbili na Watendaji wa Mahakama vilevile wana ushirikiano mzuri tu, na mimi nimepata fursa mara kadhaa kukutana nao na nashukuru na ninafurahi kusema kwamba kuna mambo mengi ambayo tunapata msaada kutoka Mahakama ya Jamhuri,” amesema Mhe. Dkt. Mwinyi.
Amesema kuwa, anatarajia kuona ushirikiano uliokuwepo ukiendelea ili kupiga hatua zaidi, na kueleza kuwa, “Sisi huku tumepiga hatua zaidi, sisi huku tumeingia katika maboresho ya miundombinu ya Mahakama, tunajenga Mahakama ngazi zote. Sasa hivi kwakweli mazingira yamekuwa mazuri zaidi kuliko miaka ya nyuma, sasa hivi mwelekeo ni kwenda zaidi katika eneo la TEHAMA, tuna imani kama wakilimudu eneo hilo maana yake mashauri yatashughulikiwa na wale wananchi ambao hawana uwezo wanaweza kupata haki kwa haraka zaidi,” amesema.
Rais Mhe. Dkt. Mwinyi amesema, Mahkama ya Zanzibar imekuwa ikipata msaada kutoka Mahakama ya Tanzania katika maeneo mengi ikiwemo matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utendaji wa Mahakama na kwamba ni eneo muhimu linalopaswa kupewa kipaumbele ili kuharakisha upatikanaji haki na kuongeza ufanisi.
“Eneo la TEHAMA ni eneo ambalo watu wetu huku wamekuwa wakijifunza sana upande wa pili na hatua mliyopiga wanataka na wenyewe waweze kufikia na wanapata ushirikiano wa kutosha,” amesema Mhe. Dkt. Mwinyi.
Amesema Mahkama ya Zanzibar ina fursa ya kujifunza kutokana na mafanikio yaliyofikiwa na Mahakama ya Tanzania katika matumizi ya TEHAMA, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati na kupunguza gharama za kiutendaji.
Aidha, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka mkazo katika matumizi ya TEHAMA na uimarishaji wa miundombinu ya Mahakama katika ngazi zote, ili wananchi wapate huduma za haki kwa wakati, katika mazingira bora na karibu na maeneo wanayoishi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo kati yake na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju alipomtembelea Ikulu Zanzibar leo tarehe 22 Juni, 2026.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi (kulia) akimsalimia na kumkaribisha Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju alipomtembelea Ikulu Zanzibar leo tarehe 22 Juni, 2026.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju leo tarehe 22 Juni, 2026 alipomtembelea Rais Mhe. Dkt. Mwinyi Ikulu ya Zanzibar.
Akizungumzia ujenzi wa miundombinu ya Mahakama, Rais Mhe. Dkt. Mwinyi amesema ujenzi wa jengo la Mahakama ya Rufani Pemba ni hatua muhimu itakayowezesha Majaji kutekeleza majukumu yao katika mazingira bora na kuimarisha huduma za kimahakama kisiwani humo.
“Lakini vilevile, kuna eneo la Ujenzi wa Miundombinu ya Mahakama, tuna Mradi mkubwa wa Mahakama Kuu kule Pemba, umefikia hatua nzuri na matarajio yetu muda si mrefu tuukamilishe ili tuweze kutoa nafasi nzuri ya Majaji wa Rufani wanapokuja upande wa pili basi wawe na mazingira ya kufanyia kazi yanayoendana na kazi wanazozifanya, kwahiyo nashukuru kwamba ushirikiano ni mzuri, mahusiano ni mazuri, kinachotakiwa ni kuyaendeleza,” amesisitiza. Rais Dkt. Mwinyi.
Ameongeza kwa kuishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kutambua kazi nzuri zinazofanywa na Serikali ya Zanzibar ambapo amesema, “Nashukuru kwamba angalau kuna jambo ambalo na sisi mmeona mjifunze kutoka kwetu, hii ni hatua kubwa kwetu kwa sababu sisi tumeshaweka hiyo ngazi ya rufaa ambayo ni fanisi zaidi kuliko ilivyokuwa awali.”
Kadhalika, Mhe. Dkt. Mwinyi amemshukuru Jaji Mkuu kwa kufika kujitambulisha kwake rasmi na amempongeza na kumtakia kila la kheri Jaji Mkuu wa Tanzania katika utekelezaji wa majukumu yake.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu amepongeza ushirikiano unaotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Mahkama ya Zanzibar.
“Mhe. Rais nashukuru kwa fursa hii ya kukuona, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kukuwezesha kuwa, Rais wetu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, yanayofanyika huku tunayaona, mwenye macho haambiwi tazama, hongera sana,” amesema Mhe. Masaju.
Aidha, Jaji Mkuu amemueleza Rais Mwinyi kuwa, amefika kumuona kwa kuwa tangu ateuliwe kuwa Jaji Mkuu alikuwa hajafika kumuona ili amfahamu na endapo ana ushauri wowote amshirikishe ili ayazingatie anapokuwa anatekeleza majukumu yake ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Nafahamu kwamba kama Jaji Mkuu pia ndio Mkuu wa Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ni Mahakama ya Muungano, yanaweza kuwepo mambo mengine ambayo ungependa kunishirikisha ili ninapotekeleza majukumu yangu nitekeleze kwa namna ambayo ni ya ufanisi sana kuimarisha muungano wetu lakini zaidi pia kuharakisha maendeleo ya Zanzibar kupitia maamuzi ya Mahakama, yaani katika kutekeleza majukumu yetu tutekeleze kwa namna ambayo hasa kwa mashauri ya Zanzibar pia yanachelewa kupata uamuzi, yapate uamuzi mapema na haki ipatikane mapema ipasavyo,” amesema Mhe. Masaju.
Jaji Mkuu amemueleza Rais Mwinyi kuwa, kwa sasa kuna vikao vya Mahakama ya Rufani vinaendelea Nchi nzima ikiwemo Zanzibar, na kwamba Mahakama ya Tanzania inashukuru kwa kupata ushirikiano mzuri kutoka kwa Jaji Mkuu wa Zanzibar na kumekuwa na mahusiano ya karibu.
“Tunajifunza mengi kutoka Zanzibar, wenzetu kuna maeneo mengine wamepiga hatua zaidi kuliko ilivyo kwa Bara na kwa mfano huku Zanzibar pia kuna Mahakama ya Mkoa, kule hakuna Mahakama ya Mkoa kuna Mahakama inaitwa Mahakama ya Hakimu Mkazi ina mamlaka sawa na Mahakama ya Wilaya, tunaona kwamba hiyo sio sawa, haiwezekani kwa mfano Mkuu wa Wilaya akawa na mamlaka sawa na Mkuu wa Mkoa na unakuta hawana kazi pale wanapangiwa kazi na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya, kwahiyo tunataka kurekebisha sheria,” amesema Mhe. Masaju.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akisisitiza jambo leo tarehe 22 Juni, 2026 alipokuwa akizungumza na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi (hayupo katika picha).Mazungumzo yakiendelea kati ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju. Aliyeketi kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Katibu wa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Venance Mlingi.
Aidha, Jaji Mkuu amebainisha kwamba, Muswada umeshaandaliwa baada ya kuwa wamejifunza kutoka Zanzibar ambapo Mahakama hiyo haitaitwa tena Mahakama ya Hakimu Mkazi bali itaitwa Mahakama ya Mkoa ili pamoja na kuwa na majukumu yake ya msingi iweze pia kusikiliza rufaa zinazotoka Mahakama ya Wilaya.
Mhe. Masaju amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Mwinyi na kusema kuwa, uamuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwa na Mahkama Kuu Pemba ni uamuzi wa Hekima na mzuri kwa sababu inawapunguzia watu umbali wa kuja kupata haki, inawapunguzia gharama, wanapata huduma katika eneo ambalo wamelizoea.
Mbali na hilo, Jaji Mkuu amesema uamuzi wa ujenzi wa Mahakama hiyo ni mzuri kwa kuwa pia eneo ambalo haki inapopatikana linapaswa lipendeze, ili mtu anapofika awe na matumaini.
Katika upande mwingine, Jaji Mkuu amezungumzia kuhusu Uchumi wa Kidijitali (Digital Economy), ambapo amebainisha kuwa, upande wa Zanzibar wao ni wepesi kuweka katika utekelezaji mambo mazuri na kuyaweka katika matumizi mapema.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi (kulia) akimsalimia na kumkaribisha Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju leo tarehe 22 Juni, 2026 alipomtembelea Rais Mhe. Dkt. Mwinyi Ikulu ya Zanzibar.
Picha ya pamoja. Kulia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi na kushoto ni Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju. (Picha na MARY GWERA, Mahakama-Zanzibar).
Ameeleza kuwa, kwa sasa wao wana Kanuni za Ushahidi wa Kieletroniki ambazo zinatumika hata katika Mahakama za ngazi za chini.
“Sasa hivi miamala mingi ya fedha inafanyika kielektroniki, na kwa Zanzibar hata Ushahidi wa Kielektroniki sasa unatumika hata Mahakama za chini kabisa kwa Ushahidi ambao watu wanaandikiana kwenye simu, kompyuta na kadhalika anaweza akautoa Mahakamani,” amesema Mhe. Masaju.
Kufuatia hali hiyo, Jaji Mkuu amesema kuwa, ameamua kuboresha Kanuni za Ushahidi za mwaka 1964 zinazotumika katika Mahakama za Mwanzo ili kuzingatia matakwa ya (Electronic Transcation) kifungu cha 19 ambacho kinaelekeza Ushahidi huo wa kielektroniki utatumika katika Mahakama zote.




