DODOMA-Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefuatilia mjadala na upigaji kura uliofanyika katika Bunge la Ulaya tarehe 18 Juni 2026 kuhusu Programu ya Ubia kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya kwa mwaka 2026 yenye Jumla ya Euro milioni 156.
Serikali imebaini kuwa baada ya upigaji kura huo, kumekuwa na taarifa mbalimbali katika
baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii zinazotoa tafsiri isiyo sahihi kuhusu
maana ya kura hiyo.
Kutokana na hali hiyo, Serikali inapenda kutoa ufafanuzi ufuatao: Kwanza, kura iliyopigwa katika Bunge la Ulaya si uamuzi wa mwisho wa Umoja wa Ulaya kuhusu Programu ya Ubia na Tanzania kwa mwaka 2026.
Kura hiyo ni sehemu ya mchakato wa ndani wa taasisi za Umoja wa Ulaya ambapo Bunge hilo limetoa maoni na mapendekezo yake kwa mamlaka nyingine zinazohusika na maamuzi ya mwisho.
Pili, kinyume na baadhi ya taarifa zinazosambazwa, mapendekezo yaliyotolewa na Bunge la Ulaya siyo kusimamishwa kwa fedha za programu za ubia zinazotekelezwa au kutarajiwa kutekelezwa nchini.
Kilichopendekezwa na Bunge hilo ni kufanyiwa mapitio Programu hiyo na kuwasilishwa tena. Aidha, kwa mujibu wa taratibu zilizopo mapitio yoyote ya programu ya ubia hufanyika kwa mashauriano na makubaliano ya pande zote mbili na hatimaye kuridhiwa kupitia Mkataba wa Pamoja wa Fedha (Joint Financial Agreement) kati ya Serikali na Umoja wa Ulaya.
Hivyo, maamuzi hayo si ya upande mmoja na hayatakuwa hivyo.Aidha, ni muhimu kwa umma kufahamu kuwa katika jumla ya Euro milioni 156 zinazozungumziwa, kiasi kilichokuwa kimepangwa kuelekezwa moja kwa moja Serikalini kupitia mifumo rasmi ya Serikali ni Euro milioni 17 pekee.
Kiasi kilichobaki cha takribani Euro milioni 139 kilikuwa kimepangwa tangu awali kutekelezwa kupitia taasisi teule za Umoja wa Ulaya, taasisi za nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya pamoja na asasi za kiraia.
Hivyo,tangu awali, sehemu kubwa ya fedha za Programu hiyo haikuwa imepangwa kuingia moja kwa moja katika mifumo ya Serikali.
Tatu, baadhi ya hoja zilizomo katika azimio lililopitishwa haziakisi kikamilifu ukweli na uhalisia wa hali halisi ya Tanzania na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na serkali baada ya matukio ya Oktoba 2025.
Serikali ilitoa ufafanuzi wa kina kuhusu hatua hizo kwa Bunge la Ulaya na kwa Wabunge wote wa Bunge hilo kabla ya upigaji wa kura.
Hivyo, Serikali inasikitishwa kwamba pamoja na ukweli huo kujulishwa, hoja zilizo katika azimio hilo hazijazingatia ukweli huo.
Serikali inapenda kuwahakikishia wananchi kuwa mahusiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Umoja wa Ulaya ni imara, ni ya kirafiki na ya kimkakati na yanaendelea kuimarika katika maeneo mbalimbali yenye manufaa kwa pande zote mbili.
Aidha, tuna mifumo rasmi ya kushauriana na kuwasiliana kwenye masuala yote yanayogusa mahusiano hayo kila kunapokuwa na hitaji hilo.


