Wizara ya Fedha yahamasisha ushiriki wa wananchi katika minada ya Serikali

DODOMA-Wizara ya Fedha imewahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika minada ya hadhara ya mali chakavu, ziada na sinzia za Serikali inayoendeshwa na Wizara ya Fedha kupitia Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali.
Wito huo umetolewa na Msimamizi wa Mali za Serikali Mwandamizi, Wizara ya Fedha, Bw. George Killo, wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, ambapo wananchi wamekuwa wakipatiwa elimu kuhusu taratibu za usimamizi na uondoshaji wa mali za Serikali.

Amefafanua kuwa, mali zinazokuwa zimechakaa, zimepitwa na wakati au kutokuwa na matumizi tena katika taasisi za umma huondoshwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo husika kabla ya kuuzwa kupitia minada ya wazi inayowapa wananchi wote fursa sawa ya kushiriki.
“Tunawahimiza wananchi kufuatilia matangazo rasmi ya minada hiyo yanayotolewa kupitia vyombo mbalimbali vya habari na mifumo ya Serikali ili kupata taarifa sahihi kuhusu aina ya mali zinazouzwa, masharti ya ushiriki pamoja na ratiba za minada husika,” alisema Bw. Killo

Aliongeza kuwa, ushiriki mpana wa wananchi katika minada ya Serikali huongeza ushindani, huimarisha uwazi katika mchakato wa mauzo na huchangia katika uongezaji wa mapato katika Mfuko wa Mikopo wa Watumishi (PSAF).

Bw. Killo, alifafanua kuwa, minada hiyo huendeshwa kwa kuzingatia misingi ya usawa, haki na uwazi, ambapo kila mwananchi anayekidhi vigezo vilivyowekwa anaruhusiwa kushiriki.

Aidha, elimu inayotolewa kwa wananchi kuhusu minada ya Serikali inalenga kuongeza uelewa wa taratibu za ushiriki na kuwawezesha kutumia ipasavyo fursa zinazopatikana.
Kwa upande wa wananchi waliotembelea Banda la Wizara katika Maonesho hayo wamepongeza juhudi za kutoa elimu kuhusu minada ya Serikali, wakieleza kuwa zimewaongezea uelewa kuhusu fursa zilizopo na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika minada hiyo kwa kuzingatia taratibu na masharti yaliyowekwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here