NA DIRAMAKINI
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Sultanate ya Oman zimeendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta ya usimamizi wa kumbukumbu na nyaraka za Serikali, kufuatia makabidhiano ya vifaa vya kisasa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Chumba cha Kanzi Data (Data Centre) pamoja na miundombinu iliyoboreshwa ya mtandao.
Akizungumza wakati wa hafla ya kupokea vifaa hivyo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema,msaada huo kutoka Mamlaka ya Taifa ya Nyaraka na Kumbukumbu ya Sultanate ya Oman ni hatua muhimu katika kuharakisha mageuzi ya kidijitali katika usimamizi wa nyaraka na kumbukumbu za Serikali.
Amesema,vifaa hivyo vitasaidia kuimarisha mfumo wa kidijitali wa usimamizi wa kumbukumbu na nyaraka za Serikali, kuongeza usalama wa taarifa muhimu za Serikali, kuboresha upatikanaji wa nyaraka kwa wakati na kuhakikisha kumbukumbu muhimu za taifa zinahifadhiwa kwa usalama na kwa muda mrefu.
"Mchango huu ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha usimamizi wa kumbukumbu na nyaraka katika mazingira ya kidijitali. Pia utasaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za umma kwa kuhakikisha taarifa muhimu zinapatikana kwa haraka, kwa usalama na kwa kuzingatia viwango vya kimataifa,"amesema Mhe. Kikwete.
Ameongeza kuwa,ushirikiano huo unaakisi uhusiano wa kihistoria na kidugu uliopo kati ya Tanzania na Oman, ambao umeendelea kuimarika katika sekta mbalimbali zikiwemo biashara, uwekezaji, utalii, utamaduni na maendeleo ya taasisi za Serikali.
Kwa mujibu wa Waziri Kikwete, uwekezaji katika mifumo ya kidijitali ya usimamizi wa nyaraka ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kujenga utawala bora, kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa Serikali za Tanzania na Oman, akiwemo Balozi wa Sultanate ya Oman nchini Tanzania, Mhe. Said Hilal Al-Shidhani, Balozi Abdallah Kilima kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, pamoja na viongozi na watumishi wa Idara ya Usimamizi wa Kumbukumbu na Nyaraka.
Tags
Habari
Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa
Kimataifa
Ofisi ya Rais-Utumishi
Ridhiwani Kikwete
Tanzania na Oman



