Ufaransa yatinga hatua ya nusu fainali Kombe la Dunia,yaichapa Morocco mabao 2-0

NA DIRAMAKINI

NAHODHA wa timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe ameendelea kuandika historia katika soka la dunia baada ya kufikisha mabao 20 katika michuano ya Kombe la Dunia la FIFA na kuwa mchezaji wa pili mwenye mabao mengi zaidi katika historia ya mashindano hayo,nyuma ya bao moja tu la kinara Lionel Messi mwenye mabao 21.
Mbappe ameiongoza Ufaransa kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia la FIFA 2026 baada ya kuifunga Morocco mabao 2-0 katika mchezo wa robo fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Boston uliopo Massachusetts nchini Marekani.

Katika mchezo huo, mshambuliaji huyo wa Real Madrid alionesha kiwango cha juu kwa kufunga bao moja na kutoa pasi ya bao (assist) moja, akithibitisha nafasi yake kama mmoja wa wachezaji wenye ushawishi mkubwa katika soka la dunia.

Mbappe alianza kupata nafasi ya kuandika jina lake kwenye orodha ya wafungaji mapema kipindi cha kwanza baada ya Ufaransa kupewa mkwaju wa penalti dakika ya 28, lakini alishindwa kuutumia baada ya kukosa penalti hiyo.

Hata hivyo, alijirekebisha dakika ya 60 kwa kufunga bao la kuongoza lililotokana na pasi ya Desire Doue, kabla ya kumtengenezea Ousmane Dembele bao la pili dakika ya 66, lililoihakikishia Ufaransa ushindi na tiketi ya kucheza hatua ya nusu fainali.

Kwa mafanikio hayo, Mbappe sasa amefikisha mabao 20 katika historia ya Kombe la Dunia la FIFA, akimkaribia Lionel Messi ambaye anaongoza kwa mabao 21, huku rekodi hiyo ikiendelea kuonesha ubora wake katika mashindano makubwa ya kimataifa.

Ushindi huo umeifanya Ufaransa kuwa timu ya kwanza kufuzu hatua ya nusu fainali, ambapo itasubiri mshindi wa mchezo mwingine wa robo fainali kati ya Hispania na Ubelgiji utakaochezwa Julai 10,2026.

Matokeo hayo yanaendeleza matumaini ya Ufaransa ya kutwaa taji la dunia kwa mara nyingine, huku Mbappe akiendelea kuwa tegemeo kubwa la kikosi hicho kutokana na uwezo wake wa kufunga na kutengeneza mabao katika nyakati muhimu za mashindano.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here