DURBAN-Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa, ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kinachofanyika jijini Durban,Afrika Kusini tarehe 6 hadi 7 Agosti 2026.
Kikao hicho ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa 46 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC unaotarajiwa kufanyika jijini Durban tarehe 17 Agosti 2026. Viongozi hao wanajadili masuala mbalimbali yanayolenga kuimarisha mtangamano wa kikanda na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika ukanda wa SADC.
Miongoni mwa ajenda zinazojadiliwa ni hali ya fedha na michango ya nchi wanachama, ripoti ya mwaka ya SADC kuhusu hali ya maendeleo ya ukanda, maandalizi ya chapisho maalumu kuhusu Brigedia Jenerali Hayati Hashim Mbita, hali ya usalama wa chakula na lishe, masuala ya jinsia, pamoja na athari za mabadiliko ya mazingira ya kisiasa duniani kwa nchi za SADC.
Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Mussa alizitaka Nchi Wanachama wa SADC kupanga na kutekeleza programu na miradi ya kikanda kwa kuzingatia vipaumbele ili kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
"Ni vyema Nchi Wanachama tukatekeleza programu na miradi yenye matokeo makubwa na yanayoonekana kwa haraka, pamoja na ile inayoweka msingi wa utekelezaji mzuri wa programu na miradi mingine, hususan katika sekta za miundombinu. Miradi hiyo inapaswa kupewa kipaumbele ili kuepusha kugawanya rasilimali chache zilizopo katika shughuli nyingi kiasi cha kupunguza ufanisi na matokeo yanayotarajiwa," alisema Balozi Mussa.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuendeleza sekta ya viwanda, kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya ukanda na kuimarisha minyororo ya thamani ya kikanda. Alieleza kuwa hatua hizo ni nguzo muhimu za kuongeza biashara ndani ya SADC na kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi wanachama.
Kwa upande wake, Balozi Tebogo Seokolo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Jamhuri ya Afrika Kusini, alitoa shukrani kwa nchi wanachama mara baada ya nchi yake kupokea rasmi Uenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa SADC.
Alisisitiza dhamira ya Afrika Kusini ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kikanda, maendeleo endelevu, amani, usalama na uchumi imara kwa manufaa ya wananchi wa ukanda wa SADC.








