Yanga SC yatinga kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu, yaivuruga JKT Tanzania

NA DIRAMAKINI

MABINGWA wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, Yanga SC wameendelea vyema na kampeni zao za msimu huu baada ya kuichapa JKT Tanzania mabao 4-0.
Ni katika mchezo wa ligi hiyo uliochezwa leo Agosti 24, 2026 katika Uwanja wa KMC, Mwenge jijini Dar es Salaam.

Ushindi huo umeifanya Yanga kufikisha pointi tisa baada ya kucheza michezo mitatu, hivyo kupanda kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.

Yanga SC inalingana kwa pointi na watani wao wa jadi, Simba SC, lakini imepata nafasi ya kwanza kutokana na kuwa na tofauti nzuri zaidi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Ushindi huo unaipa Yanga mwanzo wenye matumaini katika harakati za kutetea ubingwa wake, huku ushindani wa kuwania nafasi za juu ukiendelea kushika kasi katika hatua za mwanzo za msimu.

Mbeya City yapindua mechi

Awali,katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu uliochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, wenyeji Mbeya City waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mashujaa.

Timu hizo zilianza mchezo kwa kasi, kila upande ukilenga kupata pointi tatu muhimu, lakini hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kupata bao.

Mashujaa walikuwa wa kwanza kuvunja ukimya katika kipindi cha pili, Hijjah Shamte akifunga dakika ya 52 na kuipa timu yake uongozi.

Mbeya City haikukata tamaa na ilifanikiwa kurejea mchezoni baada ya Adilly Buha kusawazisha kupitia mkwaju wa penalti.

Dakika ya 79, Oscar Mwajanga aliifungia Mbeya City bao la pili na kuhakikisha wenyeji wanapata pointi zote tatu.

Ismail Aziz wa Mbeya City alitawazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika kipindi chote cha mchezo.

Azam FC yaishinda Pamba Jiji

Katika Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam, wenyeji Azam FC waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Pamba Jiji katika mchezo mwingine uliokuwa na ushindani mkubwa.

Azam ilianza kwa tahadhari, lakini ilifanikiwa kupata bao la kwanza dakika ya 24 kupitia Enock Molia.

Pamba Jiji haikukubali kulala na ilifanikiwa kusawazisha dakika ya 45 kupitia Nonyem Okorocha, hivyo timu hizo kwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.

Kipindi cha pili, Azam iliongeza kasi ya mashambulizi na kupata bao la pili kupitia Abdul Suleiman aliyefunga kwa mkwaju wa penalti baada ya Iddy Seleman kuchezewa madhambi ndani ya eneo la hatari.

Bao hilo lilitosha kuipa Azam ushindi wa 2-1, huku Iddy Seleman akichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

Simba yaichapa Singida Black Stars

Simba SC nayo iliendelea na kampeni zake kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Singida Black Stars katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Airtel mkoani Singida.

Simba ilianza kwa kasi na kufungua ukurasa wa mabao dakika ya 12 kupitia Clatous Chama.

Hata hivyo, wenyeji Singida Black Stars walirejea mchezoni dakika ya 22 baada ya Sheikhah Ibrahim kusawazisha na kuwapa mashabiki wa Singida matumaini ya kupata pointi katika uwanja wao wa nyumbani.

Simba iliongeza nguvu katika kipindi cha pili na kufanikiwa kurejesha uongozi dakika ya 62 kupitia Rushine De Reuck, aliyefunga bao la pili la timu hiyo.

Mchezo huo pia uliendelea kuwa na changamoto kwa Simba upande wa nidhamu ya uwanjani baada ya Anthony Mligo kuonyeshwa kadi nyekundu.

Kadi hiyo imeifanya Simba kuendelea kukabiliwa na tatizo la wachezaji wake kuoneshwa kadi nyekundu, ikiwa ni mchezo wa tatu mfululizo tangu kuanza kwa msimu ambapo timu hiyo imepoteza mchezaji kwa adhabu hiyo.

Pamoja na kucheza ikiwa pungufu, Simba ilifanikiwa kulinda uongozi wake hadi filimbi ya mwisho na kuondoka na pointi zote tatu.

Geita Gold yaanza kwa kishindo Bukombe

Katika mchezo uliovuta hisia za mashabiki kwenye Uwanja wa Kisasa wa Bukombe mkoani Geita, Geita Gold iliweka historia kwa kuanza matumizi ya uwanja huo kwa ushindi mnono wa mabao 6-2 dhidi ya Kagera Sugar.

Mchezo huo ulikuwa wa kipekee kwa timu hizo mbili, ambazo zimepanda kutoka Championship na kushiriki Ligi Kuu msimu huu.

Aidha, ulikuwa mchezo wa kwanza kwa timu hizo kucheza katika Uwanja wa Bukombe, ambao Geita Gold inautumia kama uwanja wake wa nyumbani.

Geita Gold ilianza kuandika historia hiyo mapema dakika ya 10 kupitia Richard N’gondya, kabla ya Obrey Chirwa kuongeza bao la pili dakika ya 23 kwa mkwaju wa penalti.

Yussufu Mhilu aliendeleza kasi ya wenyeji kwa kufunga bao la tatu dakika ya 34 na kuongeza jingine dakika ya 46, na kuifanya Geita Gold kutawala mchezo.

Richard N’gondya alifunga bao lake la pili katika mchezo huo dakika ya 63, kabla ya Chirwa kukamilisha siku yake nzuri kwa kufunga bao la pili binafsi dakika ya 69 na kufikisha jumla ya mabao sita kwa Geita Gold.

Kagera Sugar ilifanikiwa kupata mabao mawili ya kufutia machozi kupitia Hassan Mwatelema dakika ya 40 na Robert Mkandya katika dakika ya 90+1.

Ushindani waongezeka

Matokeo ya michezo hiyo yanaendelea kuonesha ushindani mkubwa katika Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, huku timu zikitafuta pointi muhimu katika hatua za mwanzo za msimu.

Yanga na Simba zimeendelea kuonesha ushindani katika kilele cha msimamo, huku Azam FC, Mbeya City na timu nyingine zikijaribu kujihakikishia nafasi nzuri mapema.

Kwa upande mwingine, Geita Gold imeweka alama kubwa katika mchezo wake wa kwanza kwenye uwanja mpya kwa ushindi wa mabao sita, jambo linaloipa timu hiyo na mashabiki wake matumaini makubwa katika msimu wake wa kwanza baada ya kupanda daraja.

Aidha,mfululizo huo wa matokeo unaashiria msimu wenye ushindani mkubwa, huku kila pointi ikitarajiwa kuwa na umuhimu mkubwa katika mbio za ubingwa, nafasi za kimataifa na kujinusuru na hatari ya kushuka daraja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here