BoT,BASATA,Bodi ya Filamu na Umoja wa Machifu wajadili utoaji elimu kwa umma

DAR-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) leo Agosti 18, 2026 imekutana na kufanya mazungumzo na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Bodi ya Filamu ya Tanzania pamoja na Umoja wa Machifu Tanzania, ambapo wamejadili mikakati ya utoaji wa elimu kwa umma kuhusu masuala mbalimbali yanayosimamiwa na Benki Kuu.
Kikao hicho kilichofanyika katika ofisi za Benki Kuu jijini Dar es Salaam, kilijadili uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali inayosimamia huduma ndogo za fedha, pamoja na utunzaji sahihi wa noti za Tanzania.

Hatua hiyo inafuatia mwenendo wa baadhi ya wananchi, wakiwemo wasanii na waigizaji wa filamu, kujihusisha na shughuli za ukopeshaji, ukusanyaji wa amana kupitia michezo ya ‘Upatu’ au vikundi vyingine ambavyo havijasajiliwa.

Akizungumza katika kikao hicho, Meneja wa Idara ya Usimamizi wa Huduma Ndogo za Fedha, Bw. Dickson Gama, alisema Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018 inamtaka mkopeshaji binafsi au taasisi yeyote kutojihusisha na shughuli za ukopeshaji bila kuwa na leseni ya Benki Kuu na kwa kufanya kinyume na hivyo ni kosa kisheria.

“Kifungu cha 16(1) cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018, inasema ni kosa kwa Taasisi, Kampuni na Watu binafsi kujihusisha na biashara ya kutoa mikopo bila kuwa na leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania,”alisema.
Aidha, aliwasisitiza wananchi kujiepusha na ukusanyaji wa fedha unaofanyika kiholela kwa mtindo wa michezo ya upatu au vikundi vyingine ambavyo havijasajiliwa.

Naye Meneja Msaidizi Idara ya Usimamizi wa BoT, Bw. Edwin Mtui, alitaja baadhi ya vitendo vya utunzaji mbaya wa noti na sarafu kuwa ni kukunja au kufinyanga noti mkononi, kuweka noti/sarafu katika soksi mguuni au chini ya godoro, kuweka fedha sehemu zenye uchafu au unyevunyevu, kuweka noti kwenye nguo za ndani pamoja na kuzifunga kwenye kona ya kanga au kitenge.
Aliongeza kuwa, hata vitendo vya kumwaga chini fedha katika matukio mbalimbali ya kijamii ikiwemo sherehe na kupachika noti kwenye mashada ya maua, kunachangia uharibifu wa noti hizo na ni kosa kisheria.

Alisisitiza vitendo hivyo huongeza gharama kwa Serikali kutokana na ulazima wa kuchapisha na kubadilisha noti zilizoharibika mara kwa mara, hivyo kuwataka wananchi kuwa na utamaduni wa kuzitunza noti vizuri kwa kuwa noti hizo ni tunu ya taifa.
Kwa upande wao, Kaimu Katibu Mtendaji wa BASATA, BW. Edward Buganga, Mwenyekiti wa Umoja wa machifu Tanzania, Chifu Antonia Sangalali, pamoja na Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi, Bi. Aisha Ngatila aliyemwakilisha Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, waliihakikishia Benki Kuu ushirikiano katika kutoa elimu kuhusu majukumu na shughuli mbalimbali zinzofanywa na BoT.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here